" Jamii iliyostaarabika ni yenye kuheshimu Mawazo & Mitazamo ya wengine. Mchango wako katika kazi yoyote ulenge kujenga jamii yenye Kujitambua, Kujithamini na Kujiwajibisha "

 
Friday, April 28, 2006

 Zanzibar haikukubali Muungano, ililazimishwa tu

Aprili 26, 2006 Watanzania wameadhimisha miaka 42 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wakiwa na mengi ya kujadili. Miongoni mwa mambo ambayo hivi sasa yako wazi kama ajenda zilizo huru kujadiliwa ni suala hilo la Muungano. Katika makala hii, mwandishi HAWRA SHAMTE anazungumza na Katibu wa Kwanza wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Salum Said Rashid ambaye anajulikana miongoni mwa wanaharakati wenzake kwa jina la Komredi Rashid.

Swali: Komredi unaweza kukumbuka namna nchi hizi mbili zilivyofikia hatua ya kuungana Aprili 26 mwaka 1964 na namna ninyi wa Baraza la Mapinduzi mlivyoshirikiana na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Abeid Amani Karume?

Jibu: Zanzibar katika miaka ya 60 hadi mwanzoni mwa miaka ya 70 ilikuwa ikiendeshwa na Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri na kulikuwa na ‘decree’ ya kirais (Presidential Decree) ambayo iliweka mfumo wa utawala. “Decree hii ilitaka Baraza la Mawaziri liwe linapeleka waraka wa Baraza (Cabinet Paper) kuhusu kila kitu kwa Baraza la Mapinduzi. Kwa jambo kama la Muungano ilitakiwa iwepo sheria ya kirais (Presidential Decree). Hiyo haikuwapo na hiyo ilikuwa itiwe saini na Rais na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na baadae ichapishwe katika gazeti rasmi la serikali, mambo ambayo hayakufanyika.

Swali: Sasa nini kilifanyika hata kuwezesha kuendelea kuwapo kwa muungano huo hadi hivi leo, wakati jambo hilo halikufanyika?

Jibu: Muungano upo na utaendelea kuwapo kwa sababu Muungano huo umeweza kuendelea kutokana na mfumo wenyewe. Kuna serikali mbili, ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kuna mambo ya Muungano na kuna mambo ya Serikali ya Zanzibar, usimamizi uliopo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ndio uliofanya Muungano huo uendelee kuwapo.

Chukua mfano wa ulinzi na usalama, utaona ya kwamba katika mambo 22 ya Muungano hakuna kitu kilichothaminiwa, kinachofanya kazi na kutiliwa nguvu kama suala la ulinzi kuliko la uchumi. Ndio maana utaona kila pahala katika Zanzibar kuna vyombo vya dola vya Muungano, jeshi, polisi, usalama, hizi taasisi za vyombo vya dola ndivyo vilivyofanya Muungano ukasalilia mpaka hii leo, lakini sio kuwa umeleta faida kwa Wazanzibari au hata Watanganyika, faida gani waliyopata Tanganyika hadi leo? Labda lawama!

Pale mwanzo tuliulizana huu Muungano umemletea nani tija? Umeleta tija kwa madola ya Magharibi kwa sababu wakati ule Zanzibar ilikuwa ina "strategic importance" na ilikuwa zaidi katika suala la Ukomunisti na Usoshalisti, na ule ulikuwa ni wakati wa vita baridi, na wao walikuwa na wasiwasi kuwa Serikali na Mapinduzi ya Zanzibar na Zanzibar yenyewe inaweza ikawa ndio ngome ya kupeleka Ukomunisti Tanganyika na hata Afrika nzima.

Usichukulie ukomunisti unavyoandikwa hivi leo na Magharibi kuwa umekufa, uchukulie katika mwaka 1964, kulikuwa hakuna ‘One Super Power’ kuna ‘two’ na ‘Super Power’ moja ilikuwa ikituunga mkono sisi, ya Kirusi na China na mataifa yote ya Kikomunisti. Wakati ule tulipata silaha kutoka Urusi na masuala ya usalama tulikuwa tukijifunza kutoka Ujerumani ya Mashariki (GDR).

Swali: Komredi naomba turudi nyuma kidogo kuhusu lile suala la tija, kwa vipi Muungano haukuwaletea tija Watanganyika wala Wazanzibari?

Jibu: Haukuwaletea tija Watanganyika wala Wazanzibari bali umewaletea migogoro. Tanganyika haikueleweka kimataifa kutokana na mikasa iliyotokea Zanzibar ambayo ilikuwa lazima iihami katika vyombo vya kimataifa, imeiletea migogoro kuwa mpaka leo inalaumiwa kuwa imeimeza Zanzibar, imeiletea mpaka leo migogoro kwa sababu kuna kero za Muungano, kama haziko hizo, Tanganyika isingepata tabu, isingepata lawama, kwa hiyo utaona kuwa hakuna tija kwa Watanganyika labda kwa watawala.

Tanganyika imepita katika misukosuko mingi ya kisiasa kama mataifa yote ya Afrika, lakini hata hivyo Zanzibar imepata misukosuko mingi zaidi kuliko Tanganyika na mpaka leo iko katika misukosuko kwa mfano hakuna agenda Zanzibar, leo kuna agenda ya CUF, kuna agenda ya CCM na haya ni madhara makubwa kwa Wazanzibari wote, kwa sababu kila nchi lazima iwe na agenda, wenyewe wanakubali kama Zanzibar nchi, katika fomu ya pasi ya kusafiria unaulizwa kama unataka kuandika nchi Tanzania ama Zanzibar.

Swali: Ikiwa hivyo ndivyo, unasemaje kuhusu ile kesi ya uhaini iliyomkabili Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake na mahakama ikatoa maamuzi kuwa Zanzibar si dola?

Jibu: Yule aliyetoa uamuzi ule hafahamu sheria za kimataifa. Zanzibar mpaka leo ni mwanachama wa United Nations kwa sababu haikufuta uanachama wake, kilichotokea ilifunga ofisi yake, ikachanganyisha na ofisi ya Tanganyika, hakuna utaratibu wa kujitoa katika Unietd Nations ukishakuwa umo katika 'charter' ya United Nations.

Lakini matatizo ya Zanzibar ni ya ndani si ya nje, yapo yanayosababishwa na Muungano na yapo ambayo hayasababishwi. Yanayosababishwa ni zaidi ya kiuchumi kwa sababu katika mambo 22 ya Muungano, mengi ni muhimu ya kiuchumi ambayo hayako katika madaraka ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Kwa miaka sasa hivi kuna tatizo la TRA, kuna tatizo la mafuta, SMZ ina gharama nyingi, haina mbinu za mapato, haina uwezo wa kuweka sera katika sekta ya uchumi kwa sababu mambo yote muhimu ya uchumi yako katika mambo ya Muungano, ukichukua mawasiliano, mafuta, sarafu…

Swali: Wakati hayo yakiingizwa katika makubaliano ya Muungano, wanasiasa wa Zanzibar na wataalam walikuwa hawaoni kama mambo hayo yatakuja kuleta matatizo baadaye?

Jibu: Wakati ule (1964) Wazanzibari kadhaa waliona kwamba kutakuwa na matatizo, mimi mmoja wao niliona na nikaasa sana na kukataa na nanukuliwa katika vitabu kwamba nimesema ‘inachukuliwa mamlaka na madaraka kamili ya Zanzibar na hatupati kitu chochote kile, lakini ujue yale mazingira ya wakati ule yalilazimisha hayo. Kwa sababu kwanza shauri la Muungano halikutoka Zanzibar lilitoka Tanganyika kwa sababu ilishinikizwa na Amerika na Uingereza, vitabu na magazeti yote viliandika kwamba Muungano ilikuwa project ya (Mradi wa) CIA (Shirika la Ujasusi la Marekani), kwa hiyo Muungano si project ya Tanganyika, ilikuwa project ya nje, na kwa wakati ule kwa Tanganyika, Zanzibar ni mambo ya nje na mpaka siku za hivi karibuni mambo ya Muungano yalikuwa yakiendeshwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania.

Zanzibar hakuna agenda ya ndani wala ya nje. Ndio maana Wazanzibari tunaumia, na nchi yoyote ile ambayo haina agenda haiwezi kufanikiwa, mathalan chukua uchumi, Zanzibar inanuka njaa! Je kuna mipango yoyote ya kuondoa njaa hii? Haiwezi ikawepo kwa sababu mipango hiyo lazima iwe ya kimuungano, kwa sababu mambo yote muhimu ya uchumi yako katika mambo ya Muungano. Serikali ya Zanzibar haiwezi ikasema inapunguza ushuru ili iimarishe biashara, itaambiwa si mambo yako hayo!

Swali: Unasema kwamba mlitoa ushauri, sasa ilikuwaje ikawa ule ushauri wenu haukusikilizwa?

Jibu: Mazingira hayakuruhusu, siasa ya nje ya Muingereza na Mmarekani haikuturuhusu kufanya hivyo, walitung’ang’aniza kuwa lazima tuungane.

Swali: Je unataka kusema kuwa hata Karume mwenyewe hakuwa na uamuzi juu ya hilo?

Jibu: Karume alitishwa! Hata sisi tulitishwa. Siyo Karume tu, tuliambiwa ya kwamba hapa patavamiwa, na sisi tutakamatwa na Serikali ya Mapinduzi itafutwa, na Magharibi haikubali hata siku moja kuwa Zanzibar iwe ya kikomunisti.

Haya hayakufanyika hapa tu katika ulimwengu, yalifanyika katika mataifa mengi sana, yamefanyika British Guyana, yamefanyika katika Domican Republic na nchi nyingi nyingine, siyo Zanzibar tu, katika miaka ya 50 na 60 mpaka kumalizika ukomunisti, mataifa madogo ya ulimwengu wa tatu na hata mataifa madogo ya Ulaya yalikuwa yakiishi katika hali ya hatari, hali ya wasiwasi, hayawezi yakawa na sera zao wenyewe kama leo unavyoona, lazima watu wafuate IMF, lazima wafuate World Bank na wakati ule ilikuwa lazima wafuate ubepari.

Swali: Sasa ikiwa walikataa Zanzibar isiwe nchi ya Kikomunisti, lakini baada ya miaka michache tu baada ya muungano, 1967, Mwalimu Nyerere akaifanya Tanzania ikawa nchi ya Kisoshalisti?

Jibu: Walimpinga. Walilipinga Azimio la Arusha. Nyerere alitoka mrengo wa kulia akaingia wa kushoto kwa sababu wakati ule marafiki wa Afrika walikuwa Wakomunisti na maadui wa Afrika walikuwa Wakepitalisti, ukichukua suala la ukoloni, hakukuwa na koloni la Mashariki katika Afrika, kulikuwa na makoloni ya Magharibi, halafu katika vita vya kumuondoa mkoloni waliounga mkono ni mataifa ya Mashariki, siku zile vita vilikuwa vikipiganwa kwa silaha katika Afrika, waliokuwa wakitoa silaha ni mataifa ya Mashariki, waliokuwa wakifundisha watu kupigana ni mataifa ya Mashariki, kwa hivyo Mwalimu hakufanya makosa aliposema kwamba marafiki zake wa kweli ni mataifa ya Mashariki.

Swali: Unasema kwamba walimpinga Mwalimu Nyerere, kwanini wasimtishie kama walivyoitishia Zanzibar?

Jibu: Kwa sababu yeye hakuwahi kusema ni Mkomunisti, alisema yeye ni mjamaa, tena Ujamaa wa Kiafrika kama wa Leopard Sengo ambaye ndiye aliyeanzisha ‘African Socialism.’

Walimpinga kwa sababu alifilisi mali yao, mabenki yao, viwanda vyao, mashirika yao ya bima, madini yao, mali yote ya Magharibi yalifilisiwa, lakini leo si yamerudi palepale?

Swali: Tumeshaona historia na sababu za kuwapo kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, sasa tufanye nini ili kuimarisha huu Muungano ambao pamoja na kuwapo kwake kwa utatanishi lakini kila mtu anaona kwamba umeleta faida zaidi kuliko hasara?

Jibu: Sisi tulivyokuwa tunagombania Uhuru, lengo letu lilikuwa umoja wa Afrika na tulifahamu umuhimu wa kuungana na ushahidi wa umuhimu wa kuungana unaonekana dhahiri hivi sasa, kwa sababu Afrika haikuungana. Kuna matatizo Afrika nzima na haya hayataondoka mpaka Afrika iungane, kwa hiyo huu Muungano, ukiuchukulia kama chanzo cha Umoja wa Afrika, ni kitu cha maana sana, kama kuna haja au hakuna haja ya Muungano kama ulivyo mfumo wake hivi sasa hilo ni suala jingine.

Umeuliza kifanywe nini. Cha kufanya sasa hivi wakati tuna miaka 42 ya Muungano, kila Mtanganyika, Mzanzibari afanye tathmini, amepata faida gani yeye binafsi katika Muungano huu katika hii miaka 42? Acha lile tabaka tawala, la Tanganyika na la Zanzibar, wananchi wa kawaida wamepata faida gani? Watanganyika wamepata faida gani, Wazanzibari wamepata faida gani? Vipi wanaweza kupata faida katika Muungano? Kwa mfumo upi? Hili ni suala la watu wote, lakini kwa fikra zangu mimi, kunatakiwa tathmini ya haraka sana ambayo ifanywe kwa uwazi na watu wote washirikishwe hasa hapa Zanzibar kwa sababu Tanganyika haikumezwa, iliyomezwa ni Zanzibar.

Kwa hivyo hili suala ni muhimu zaidi hapa Zanzibar kuliko Tanganyika, halafu usisahau kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Muungano ndiyo Serikali ya Tanganyika, kwa hivyo Tanganyika imeongezewa madaraka na Zanzibar imepunguziwa madaraka katika huu mfumo wa Muungano.

Ingawa watu wanailaumu SMZ katika sekta ya uchumi lakini haina nguvu, watafanya nini? Hawawezi wakakaa wakaita wataalam wa mambo ya uchumi, kuwapangia mipango ya kuendesha uchumi wa Zanzibar kwa sababu mambo yote ya uchumi ni mambo ya Muungano, hilo ndilo tatizo kubwa lililomo katika Muungano. Ikiwa mambo haya hayatarekebishwa matatizo hayatakwisha, tatizo kubwa ni kuwa hakuna agenda Zanzibar na hiyo ndiyo sumu inayowaua taratibu Wazanzibari.

Swali: Unasema kwamba Tanganyika haikumezwa iliyomezwa ni Zanzibar, lakini kuna maneno yanayosemwa kwamba Zanzibar wamenufaika zaidi na Muungano kuliko inavyonufaika Tanganyika kwa sababu Wazanzibari wanapata fursa zaidi ya kufaidi matunda ya Muungano kuliko wanavyopata Watanganyika.

Jibu: Hiyo inaeleweka, kwa sababu Nyerere, mwenyewe aliliona hilo lakini kwa kuwa Tanganyika ni kubwa sana kuliko Zanzibar ni lazima aliye mdogo apate ‘prevelages’ fulani ambazo hawezi kupata mkubwa, ili ile dhana ya samaki mkubwa kummeza mdogo isije ikashika mashika.

Lakini mfumo wa Muungano wa wakati ule tofauti na wa leo, wakati ule Karume alikuwa na madaraka, alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, halafu kulikuwa na vyama viwili, Zanzibar chake na Tanganyika chake (TANU na ASP), ulipokuja utaratibu wa chama kimoja tena ndicho chenye madaraka ya mwisho, utaratibu huo ulitumika vibaya sana kuondosha madaraka kutoka Zanzibar kuyapeleka katika Jamhuri ya Muungano na mambo mengi yalipitishwa wakati huo.

Hata ile Katiba ya Muungao ilipokuja haikuja katika utaratibu uliowekwa katika hati iliyotiwa saini na marais wawili kwa sababu ilitakikana liitwe Bunge la Katiba, halikuitwa Bunge la Katiba.

Swali: Sasa Bunge hilo la Katiba lingeitishwa vipi kwa pande zote mbili wakati Zanzibar hakukuwa na Bunge?

Jibu: Kwa mujibu wa ‘Presidential Decree’ namba 3 iliyotiwa saini na Karume na mimi kama Katibu wa Baraza la mapinduzi, ilikuwa lazima uitwe uchaguzi mwaka mmoja baada ya Mapinduzi na ile hati ya Muungano ilikubaliwa liitishwe Bunge la Katiba mwaka mmoja baadaye ili kutathmini na kupasisha Katiba ya Kudumu ya Muungano na uchaguzi Zanzibar ulikuwa ufanyike Januari 1965, lakini yote hayo hayakufanyika.

Hapa pana mambo mawili, kuna sheria na kuna hali halisia ya mambo yalivyo, tukubali, tusikubali, Muungano upo, umeendelea miaka 42 na hakuna ishara ya kuonyesha ya kwamba utatoweka!

Swali: Sasa tufanye nini ili kuondosha hizo zinazoitwa kero za Muungano?

Jibu: Vipi Wazanzibari washirikishwe katika kuondosha kero hizi. Kwanza SMZ lazima izishughulikie, hasa Rais wa Zanzibar kwa sababu huu Muungano ulikuwa kati ya Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar, pahala pazuri sana ni rais wa Muungano na Rais wa Zanzibar kuzishughulikia kero za Muungano. Kwa upande wa Tanganyika kuna utaratibu, kwa upande wa Zanzibar utaratibu unaofaa ni kuwashirikisha Wazanzibari wote na kufahamishwa, kuelezewa ili sote tuwe na agenda ya Zanzibar, nikisema hivyo namaanisha kwamba chama kilicho katika madaraka na chama cha Upinzani, juu ya suala hili wasiwe na mgogoro na uhasama na uadui kwa sababu linawahusu watu wote.

Swali: Lakini lipo tatizo jingine la kuwa hali ya Zanzibar kuwa ni dola ama si dola.

Jibu: Zanzibar unaweza kusema ni ‘sovereign’ na si ‘sovereign’. Kisheria Zanzibar ‘sovereign’ na inaweza leo ikadai ile ‘sovereignty’ yake. Mwalimu Nyerere aliwahi kumwambia Colen Legarb wa ‘London Observer’ (1965) kwamba ikiwa Wazanzibari watataka kuuvunja Muungano, sitawapelekea majeshi ‘I will not bomb them’ (anamnukuu alivyosema Nyerere), Mwalimu kama mwasisi wa Muungano alijua kwamba Karume alikuwa akiliwakilisha taifa iliyo huru, wala Zanzibar haikutekwa kijeshi na Tanganyika, wala kihistoria Zanziabr katika karne 4 zilizopita haijapata kuwa sehemu ya Tanganyika, ingawa Tanganyika ilipata kuwa sehemu ya Zanzibar lakini Zanzibar haijapata kuwa sehemu ya Tanganyika. Ufalme wa Zanzibar ulikuwa ukitawala takriban katika ufukwe wote wa Afrika Mashariki ikiwemo Dar es Salaam, Kilwa na kwengineko halafu Mjerumani akainunua Tanganyika kutoka Zanzibar na akaitawala, lakini nawaomba Watanganyika wasiwe na chuki na Zanzibar kwa mambo yaliyopita. Haina haja ya chuki, sisi ni mataifa pacha, Tanganyika na Zanzibar, sisi tunapenda Muungano uendelee na haiwezekani Zanzibar ikakaa katika uhasama au ikaihatarisha Tanganyika, itakuwa tunajihatarisha wenyewe.

Maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Rufaa Tanzania ninavyoitafsiri mimi ni kuwa ikiwa ukitaka kupindua ni lazima upindue Serikali ya Muungano, huwezi ukapindua Serikali ya Zanzibar.

Swali: Kwanini isiwezekane kupindua Serikali ya Zanzibar wakati ina Rais wake na chombo vyake vya kutunga sheria, kwanini isipinduliwe?

Jibu: Kwa sababu mpaka leo haina utambulisho wa kimataifa. Ikiwa tutakubaliana kwamba kuna faida kubwa ya kuwa na viti viwili kuliko kimoja katika Umoja wa Mataifa kwa upande wa Tanzania, kesho Zanzibar itampeleka mtu kama Balozi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa.

Swali: Ilikuwaje Zanzibar ikakubali kunyimwa haki zote hizo?

Jibu: Hii nakurudisha tena pale kutokana na mazingira ya wakati ule. Kwa nini Zanzibar ilikubali kutawaliwa na Mwingereza mwaka 1890, Kwa nini katika mwaka 1808 ilikubali kutawaliwa na Ujerumani? Kwanini Afrika ilikubali kugawanywa na kutawaliwa na wakoloni? Huwezi kusema kuwa ilikubali, ililazimishwa kukubali mipango ile.

Swali: Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete alisema kwamba muundo wa Muungano hauna matatizo, bali wenye matatizo ni viongozi, je wewe unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Mimi naona hili suala la viongozi muhimu sana, lakini itakuwa makosa kama viongozi watakaa kwenye vikao vya siri kuyatatua matatizo haya, hayataondoka, haya matatizo yanawahusu wananchi, hayawahusu viongozi. Vilevile Rais Kikwete ameagiza Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wakutane hata kama hakuna matatizo. Ikiwa Jaji Nyalali na Jaji Kisanga wameona kama kuna matatizo. Walizungumza na watu wengi na walichukua muda mrefu na kuona kuwa una matatizo.

Nadhani iko tofauti kubwa kati ya awamu ya Kikwete na zile zilizopita, angalau yeye anazungumzia kuwa kuna kero, pia amesema kuwa suala la Zanzibar linategemea Wazanzibari wenyewe. Suala la Zanzibar liko namna mbili; Huwezi ukatatua migogoro ya kisiasa ndani ya nchi ukapata maendeleo peke yake bila kutatua kero za Muungano, haiwezekani, hayo mambo mawili yanakwenda sambamba. Suala siyo Serikali mbili au tatu, suala ni madaraka na mamlaka ya Serikali, leo yakipunguzwa mambo ya Muungano yakarudishwa kwenye SMZ, mambo katika sera za sekta za uchumi na pakawepo Zanzibar suluhu ya kisiasa kati ya watu wanaogombana, wenye uhasama na uadui hali inayosikitisha hasa ukizingatia kwamba hawa ni ndugu. Ikiwa Zanzibar kuna agenda na kuna mipango ya kiuchumi katika miezi 18 tu hali ya maisha Zanzibar yanaweza yakabadilika.

Swali: Kwa hiyo unasema kuwa tatizo kubwa la Wazanzibari katika Muungano ni uchumi zaidi kuliko siasa?

Jibu: Unajua sisi ni nchi ndogo, na hatuna ‘ambitious’ zile za kutawala na ‘ku-influence’ hatuwezi, hata kama tukitaka. Zaidi kitu ambacho kingetushughulisha sasa hivi ni kula yetu, ajira kwanza, halafu tukishakuwa katika hali nzuri na tunaendelea ndio masuala hayo ya Serikali ngapi yafuate.

Kuna mambo mengi Zanzibar imenyang’anywa. Ziko ‘economic and financial consequenses’ za Muungano. Kwa mfano mpaka leo suala la ‘currency board’ ya Afrika Mashariki halijamalizika. Kuna fedha za Zanzibar ambazo mpaka leo haijazipata kutoka Serikali ya Muungano, itabidi zifanyiwe hesabu za miaka 42 ili tujue nani kapata faida na nani hakupata.

Swali: Wapo wanaosema kuwa matatizo ya nchi masikini zinazoendelea ni ulafi wa viongozi tu, je dhana hiyo ina ukweli kiasi gani?

Jibu: Mimi nafikiri matatizo yanatokana na mifumo ya kiutawala si ulafi wa viongozi, ile mifumo ambayo inawafanya watu kama hao wakawa viongozi, watu walafi, wala rushwa na wasio na uzalendo, watu wanaojipigania maslahi yao kwa kurundika mali na kujibeparisha na wasiojali maslahi ya umma. Ikiwa katiba inampa nafasi Rais kusema ‘serikali yangu’ huoni kama hiyo ni hatari! Ikiwa itatokea nafasi ya kubadilisha katiba hapa Zanzibar, tunapaswa tuwe makini sana ili taasisi zisiweze kutengeneza madikteta.

Lakini nchi yoyote ile ambayo watu wamegawanyika kama tulivyogawanyika sisi hapa Zanzibar, ikawa kuna uadui na uhasama kati ya pande mbili zinazoleta mtafaruku wa kisiasa, maslahi yake hupotea, nchi ambayo haina umoja wa kitaifa haiwezi ikasimamia maslahi yake.

KUHUSU MIMI

JINA:Hawra Shamte
MAKAZI:Dar es salaam
NCHI:Tanzania
KAZI:Mwandishi

KUELEKEA BUNGE LA BAJETI 2006

QuickTopic free message boards
Bonyeza hapa ili uweze kuelezea: NINI MTAZAMO WAKO JUU YA BAJETI IJAYO YA MWAKA 2006/07 NCHINI TANZANIA?

VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI

  • The Citizen
  • Mwananchi
  • Mwanaspoti
  • Business Times
  • Majira
  • Daily News
  • Nipashe
  • The Guardian
  • The Express
  • Kiongozi
  • Uhuru/Mzalendo
  • Arusha Times
  • BLOGI ZA KISWAHILI

  • Bangaiza
  • Mwandani
  • Pambazuko
  • Damija
  • Mtafiti
  • Martha
  • Gaphiz
  • Swahili time
  • Miruko
  • Dira yangu
  • Msangimdogo
  • Jeff Msangi
  • Kasri la mwanazuoni
  • Kurunzi
  • Baragumu
  • Mawazohuru
  • Fikra Thabiti
  • Mtandaoni
  • Motowaka
  • Mkwinda
  • Ngurumo
  • Nyembo
  • Bwaya
  • Omega
  • Tafakari za Maisha
  • Nuru akilini
  • Mtandawazi
  • Mhujumu
  • Vijimamboz
  • Wakati wa Ukombozi
  • Kijiwe Joto
  • Watoto Wetu
  • Jungu kuu
  • Kisima cha Weledi
  • Jarida la Ughaibuni
  • Bhalezee
  • Sauti ya Baragumu
  • Kona yangu
  • Furahia Maisha
  • Bakanja
  • Terrie Swai
  • Fatma Karama
  • Kazonta
  • Binti Afrika
  • Blogu ya Kilimo
  • Ukombozi
  • Mwafrika
  • Digital Africa
  • Blogu ya lugha mseto
  • BLOGI ZA WAAFRIKA

  • BLOGAFRICA
  • BLOGU ZA WAAFRIKA
  • DIGITAL AFRICA
  • MAMA JUNKYARD'S
  • MSHAIRI
  • KENYAN PUNDIT
  • MONGI DREAMS
  • ISARIA MWENDE
  • CUNNING LINGUISTICA
  • ETHIOPUNDIT
  • MOCHALICIOUS
  • UNGANISHA
  • DEMOKRASIA KENYA
  • CHANUKA
  • BANKELE
  • MAARIFA/AKIEY
  • AFROMUSING
  • NEHANDA DREAMS
  • BLACK LOOKS
  • YUMMY WAKAME
  • AFRICAN OIL POLITICS
  • NUBIAN SOUL
  • SANAA
  • VIRTUAL INSANITY
  • MENTAL ACROBATICS
  • KENYA UNLIMITED
  • JIKUMBUSHE KAZI ZANGU ZA ZAMANI

    April 2006 May 2006 June 2006 October 2007 November 2007 December 2007 May 2008 July 2008 October 2008 July 2009 August 2012 October 2012

    Imetengenezwa na

    Ukibofya hapa utapelekwa katika Blogi ya msangimdogo

    na inawezeshwa na