" Jamii iliyostaarabika ni yenye kuheshimu Mawazo & Mitazamo ya wengine. Mchango wako katika kazi yoyote ulenge kujenga jamii yenye Kujitambua, Kujithamini na Kujiwajibisha "

 
Wednesday, July 22, 2009

 Waislam, jukumu la kuanzisha Mahakama ya Kadhi ni lenu

WIKI iliyopita wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni alisema kwamba serikali haijalitupa suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, lakini imependekeza kuwa kutokana na suala hilo kuwa la imani, liundiwe mfumo wake ambao hautasimamiwa na dola ili chombo hicho kiendelee kuwa nguzo muhimu ya dini ya Kiislamu.

Pinda amesema kwa kuwa Mahakama ya Kadhi ni suala la imani, hivyo Waislam waiunde katika mfumo wao na serikali itatoa msaada kwa chombo hicho hadi kitakaposimama.

Amesema chombo hicho kikiundwa na kusimamiwa na dola serikali itakuwa inakiona kama chombo chake cha dola tu hivyo haitakuwa imetenda haki kwa Waislam na hata Watanzania kwa ujumla wao.

Waziri Mkuu amesema kwa kuwa inasemwa kwamba Mahakama ya Kadhi, au ofisi ya Kadhi msingi wake ni imani ya dini, hivyo anadhani si busara chombo hicho kikawekwa katika mfumo unaotakiwa kusimamiwa na dola.

Kwa kauli hiyo ya Waziri Mkuu ni wazi kwamba Waislam sasa wanapaswa kukianzisha chombo hicho wao wenyewe na kutafuta utaratibu mwafaka wa kuzifanya sheria na maamuzi yake yakubalike na jamii ya Waislam nchini Tanzania.

Binafsi nakubaliana kwa asilimia 100 na tamko hilo la Waziri Mkuu Pinda, kwani ni wazi kwamba serikali itakapoianzisha mahakama hiyo itabidi iwe ni miongoni mwa vyombo vya serikali na itakayosimamiwa na serikali yenyewe na wala si Waislam.

Serikali mwaka 1968 iliivunja Jumuiya ya Kiislam iliyoitwa East African Muslim African Society (EAMWS) jumuiya iliyoanzishwa na Agakhan na ambayo viongozi wake wengi walikuwa ni wenye asili ya Kiasia. EAMWS kama jina lilivyo ilikuwa ni jumuiya ya Waislam ya Afrika Mashariki.

Baada ya kuona kuwa Waislam wa Tanzania kwa ujumla wao hawawakilishwi vema na EAMWS na kutoa malalamiko kadhaa wa kadhaa, ndipo serikali ilipoifuta jumuiya hiyo na kuwahamasisha viongozi Waislam waliokuwa Serikalini kusimamia kuanzishwa kwa jumuiya nyengine ya Waislam wa Tanzania. Kwa msaada wa Sheikh Abeid Karume na Sheikh Rashid Kawawa waliwakutanisha masheikh wa Kiislam pale Iringa mwaka huo huo 68 na kuanzisha Baraza Kuu la Waislam Tanzania, na kwa kuwa EAMWS ilivunjwa kisheria, mali zote zilizokuwa za EAMWS zilimilikishwa BAKWATA.

Kutokana na insafu hiyo, BAKWATA kwa Waislam ikawa inaonekana kuwa ni chombo cha serikali japokuwa serikali haiwachagulii kiongozi wala haiwalipi mishahara isipokuwa hutoa msaada pale inapoombwa kufanya hivyo.

Kutokana na iktisadi hiyo na pengine matendo yasiyoridhisha au yasiyoisaidia jamii ya Kiislam kwa ujumla wake nchini, ndipo mara baada ya kufunguliwa milango ya mfumo wa kiliberali na ruhusa ya kuanzishwa kwa vyama vya kijamii katika miaka ya 1980, ndipo jumuiya nyingi za Kiislam zikaibuka kama uyoga. Nia ikiwa kuziba mapengo pale ambapo Bakwata imeshindwa na pengine kuwafanya Waislam wawe wamoja zaidi.

Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislam mathalan, lililoanzishwa kwa jitihada za wasomi na masheikh mbalimbali wasiokubaliana na mawazo na matendo ya Bakwata, ilidhaniwa kuwa hilo lingeweza kujenga jumuiya yenye nguvu na kuwaunganisha Waislam wawe na sauti moja. Hadi leo Baraza hilo lina umri wa miaka 15 na bado halijapiga hatua, ndio kwanza linasimama dede na wala jitihada zake za kuunganisha jumuiya na taasisi za kiislam hazijafanikiwa kihivyo.

Jitihada nyingine za Waislam za kuwanyang’anya Bakwata mamlaka yao kwa Waislam nchini, walianzisha Baraza la Misikiti Tanzania (BAMITA). Baraza hilo hadi sasa limebakia Kisarawe tu. Waislam wanapaswa kujiuliza kwanini jitihada zao zinasuasua, watafute mbinu za kujikwamua na waache kuwanyooshea wengine vidole?

Hoja iliyopo ni kwamba ikiwa Waislam hawaipendi Bakwata kwa madai kuwa ni kibaraka wa serikali, itakuwaje kwa Mahakama ya Kadhi endapo itaundwa na kuingizwa katika mfumo wa Serikali? Je, itakuwa ni chombo cha Waislam au chombo cha Serikali?

Binafsi nadhani Waislam walikokotwa na ahadi za kisiasa zilizoanza kutolewa na Augustine Mrema wakati akiwa NCCR Mageuzi na baadaye hoja hiyo kupokwa na CCM. Ukiiangalia kwa undani wake utaona kuwa ni hoja ya kisiasa tu ambayo hujengwa kwa maslahi ya wakati fulani.

Kadhalika kuna madai ya kwamba zipo nchi zenye ofisi ya Kadhi Mkuu na Mahakama ya Kadhi ambazo zinasimamiwa na Serikali, hiyo ni kweli lakini ukiangalia utakuta kwamba idadi ya Waislam katika nchi hizo ni ndogo, hivyo serikali inachofanya ni kulinda haki za wachache (minority rights) lakini katika nchi kama Tanzania ambayo takribani idadi ya Waislam na wasio Waislam inakaribiana, kuunda chombo cha kisheria kitakachosimamiwa na dola kwa maslahi ya dini moja pengine ni hoja yenye ukakasi kidogo.

Ni kweli iko haja ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na ofisi ya Kadhi Mkuu nchini Tanzania lakini si haki kuishinikiza serikali kuanzisha mamlaka hizo, Waislam wenyewe wanapaswa wazianzishe na kuzisimamia, wanachopaswa kuitaka serikali kufanya ni kuzitambua tu kisheria na kutoa msaada pale inapohitajika.

Hata hivyo swali linalojitokeza ni kuwa ni nani atakayemfunga paka kengele? Swali hilo linakuja kwa sababu nchini Tanzania Waislam hawana mamlaka moja wanayoiamini na kuitegemea kusimamia mambo yao, Waislam wamegawanyika si kwa madhehebu tu bali kwa makundi na kwa taasisi mbalimbali ambazo kimsingi nyingi hazikubaliani kimtazamo.

Hawra Shamte ni mhariri wa siasa wa gazeti la Mwananchi.
hshamte@mwananchi.co.tz
0754 849694

Tuesday, July 14, 2009

 Mzimu wa Muungano tusipoutuliza utatukosesha amani

MAFAHALI wawili wakipigana ziumiazo nyasi. Huo ni msemo maarufu wa Kiswahili ambao bila shaka una maana pana. Hivi sasa hapa kwetu kuna mafahali wawili wapiganao, yeyote yule atakayebwagwa au hata ikiwa kila mmoja mwisho wa siku atashika njia yake, lakini ni wazi kwamba nyasi zitakuwa zimegaragazwa. Suala la mafuta ambayo yanadaiwa kuwapo Zanzibar limegeuka mzimu unaokuja na kuondoka, lakini hivi sasa unaonyesha kana kwamba umeamua kubaki kwetu, unatukokoteza, unaturudisha nyuma, unatutia wahka. Kwa kawaida mzimu wowote hutulizwa, hivyo ili na huu usiendelee kutuandama tunapaswa kutafuta njia za kuutuliza, kinyume cha hivyo utatukosesha amani. Suala hili limekuwa likiibuka mara kwa mara kwa sababu tu kwa muda wote limekuwa likishughulikiwa kwa udanganyifu, inaonyesha kana kwamba katika kamati ya kushughulikia kero za Muungano inayoongozwa na Makamu wa Rais wajimbe wakiwemo, Waziri Mkuu kwa upande wa Bara na Waziri Kiongozi kwa upande wa Zanzibar, kuna watu ambao wanaogopana, au labda kuna upande unaouogopa mwingine na kushindwa kuambizana ukweli na kinachobaki ni kutoa ahadi za kisiasa tu zisizo na mwisho, “suala hili tunalishughulikia,” siku zinakwenda, miezi inapita, miaka inakatika, awamu zinabadilika, ahadi hiyo bado ingalipo. Mara hii Wazanzibari wameamua kumtafuna jongoo kwa meno. Kasimama Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mansour Yusuf Himid mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Mkuu wa Shughuli za Serikali ndani ya Baraza, Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha akiwapo na akiwa kimya kumsikiliza. Kwa sauti kubwa na ya hamasa, Himid akasema ‘Wazanzibari tumechoka kuburuzwa katika suala hili, sasa huu ni uamuzi wa Baraza la Mapinduzi kwamba mafuta tunayatoa rasmi katika mambo ya Muungano…” Kiongozi wa mambo ya Serikali Barazani yuko pembeni kaketi, kimya kanyamaza, anang’aa ng’aa macho tu. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba Himid kapata baraka zote kutoka kwa wakuu wake kulisema jambo hilo, maana yake ni kwamba sasa watu wanataka kupimana nguvu. “Hii ni serikali ya Mapinduzi ati! Ikiwa hawa wenzetu hawataki kuelewa hivyo, itabidi sasa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itumie uamuzi wa nchi za kimapinduzi katika kuliondoa suala la mafuta na gesi asilia kwenye orodha ya mambo ya Muungano…” Bara nako wakubwa wanasema yao, eti Wazanzibari wanajifurahisha, eti mwenye mamlaka ya kutoa jambo katika Katiba ya Muungano ni Bunge tu. Hee! Kasheshe!Mara hii hapatoshi! Huenda pakachimbika bila sululu. Wazanzibari sasa wameamua kulishughulikia suala la mafuta na pengine mambo mengineyo yaliyoongezwa katika orodha ya mambo ya Muungano kutoka kumi na moja hadi 22, ilikuwaje yakaongezwa? Kwa idhini ya nani? Katika vikao vipi? Hayo ni maswali yanayoulizwa na bado hayajapata majibu labda kwa sababu hakuna mjibuji au hayajibiki. Wazanzibari sasa wanasema katika hili watatumia ukaidi, na kwa ukaidi hawajambo! Kwa ubishi kama wenyeji wa Kigoma, ubishi wao hawishi, wako tayari kukata kole la mnazi ili kuhesabu nazi zilizomo kwa sababu walishindana idadi yake wakati kole likining’inia mnazini, sasa kupata uhakika ni lazima liangushwe ili nazi zihesabiwe watu wote wakiona, huo ndio ukaidi wanaotaka kuuanzisha Wazanzibari na kwa hili husahau tofauti zao za kisiasa, hivi sasa itikadi yao moja tu, Uzanzibari na haki yao katika Muungano, likimalizika hili wataurudia ubishi wao wa zamani ule wa CCM na CUF waliouweka pembeni. Hali hiyo inaonyesha kwamba viongozi wetu wameshindwa kulishughulikia suala hili, lakini kwa kuliacha hivi lilivyo kwa kila mwenye kinywa, sauti na nafasi kusema atakavyo, huenda lisitufikishe popote na badala yake kuzua mgogoro mkubwa au pengine tuseme kwamba sasa mgogoro wa kikatiba utaibuka na hautazimika mpaka zijulikane mbichi na mbivu. Mara kwa mara wataalamu wa masuala ya siasa wamekuwa wakipendekeza kwamba tatizo hilo lianze kutatuliwa katika chanzo chake na si katika matawi, tatizo ni Katiba na Mkataba wa Muungano au pengine tatizo ni Muungano wenyewe. Inashangaza kuona kwamba watawala hawataki na wala hawapendi mambo haya yaguswe, lakini ni vyema yakaguswa na kuzungumzwa leo kuliko kusubiri mpaka ukaidi na mabavu yatumike kwani kwa kuruhusu hayo kutokea, huenda tukagawana mbao! Hiyo ni kuonyesha kwamba subira ya wananchi wa Zanzibar sasa inakaribia kufikia kikomo na hiyo inadhihirishwa kutoka vinywani mwa wawakilishi wao, haya mambo si ya kuyafanyia mzaha kwani Waswahili wanasema; ‘Mzaha mzaha, hutumbuka usaha.’ Binafsi nadhani mpira huu wa masuala ya Muungano sasa unapaswa kuchezwa na wakuu wa nchi husika, wasiachiwe Mansour Himid na Adam Malima kurushiana pasi kali na kuziumiza nyasi, kwani hawa ni vijumbe tu, tunawaomba wahusika waingie uwanjani walisakate kandanda! Hawra Shamte ni Mhariri wa Siasa wa Gazeti la Mwananchi. hshamte@mwananchi.co.tz 0754 849694

Labels:

 Fikra pevu kamwe haitakufa

NI vigumu kuamini, lakini ni kweli, wakati wake ulifika, aliitwa naye akaitika. Atakumbukwa kwa mengi mazuri, hasa kwa mchango wake kwa jamii. Mpiganaji wa haki za binadamu na msema kweli.

Profesa Haroub Othman Miraji (68) ni vigumu kwa anayemtambua kuamini kuwa ametutoka, amekwenda kwenye pumziko la milele. Ingawa binadamu hapendi kuamini linapomtokea linalomuhuzunisha, au kwa vile ana tabia ya kupenda kusikia yale yanayompendeza tu, kifo cha Profesa Haroub kilitufanya wengi kutoziruhusu akili zetu kukubali ukweli, lakini bado ukweli unabaki pale pale, kwamba pamoja na kuwa tulimhitaji lakini Mungu alimhitaji zaidi, wakati wake ulifika, aliitwa na akaitika.

Kama mpigania haki mashuhuri wa Afrika Kusini Steven Biko alivyowahi kusema kwamba ‘fikra njema ni ile isiyokufa na ni vema kufa kimwili kuliko kufa kifikra,’ fikra na mawazo ya Profesa Haroub yatadumu milele, ulioondoka kwetu ni mwili tu lakini fikra zake zitabaki kuwa hai kwa wanamapinduzi na wapigania haki za wanyonge.

Profesa Haroub ni alama ya fikra pevu, mahiri na yenye busara. Pamoja na wadhifa aliokuwa nao na heshima katika jamii lakini alikuwa mtu wa watu, tayari kuzungumza na kila aliyemkabili, hakubagua mdogo wala mkubwa, kwake yeye mwenye elimu na asiyekuwa na elimu hakuwa na tofauti katika misingi ya kibinadamu.

Aliamini kwa dhati kwamba binadamu wote ni sawa, hakujikweza wala hakutakabari. Binafsi Profesa Haroub alikuwa ni chanzo changu cha habari (source). Kila ninapotingwa na jambo hasa katika masuala ya siasa, mitafuruku na migogoro yake, Profesa Haroub ndiye aliyekuwa kimbilio langu, simu moja tu ilitosha kupanga naye miadi ya kufanya mahojiano na kama hayupo nchini atakwambia ‘niandikie maswali unitumie mtandaoni.’ Ukimwambia muda wa mwisho wa kuwasilisha, hakikisha kwamba majibu yako utayapata ndani ya muda mulioahidiana. Ukimwambia nitakuja ofisini kwako saa tatu asubuhi, saa tatu kasoro robo yeye atakuwa ameshafika.

Profesa Haroub alikuwa mahiri katika kudadavua suala la kisiasa Zanzibar na pia alikuwa rejea muhimu katika masuala ya katiba na sheria. Bila kigugumizi Profesa Haroub siku moja aliniambia kwamba ‘Katiba ya Tanzania imejaa viraka,’ nami nikaandika hivyo katika makala. Hata hivyo hakuishia hapo ila alivieleza viraka vingi vilivyomo katika katiba na kisha kutoa ushauri. Alisema kwamba kama nguo imejaa viraka kweli yaweza kuvalika? Uking’ang’ania kuivaa bila shaka siku moja itakuadhiri. Akaendelea kusema kwamba nguo yenye viraka vingi inapoteza uhalisia wake, inapoteza taswira yake ya awali, hivyo kama uliupenda mshono wake ni vema ununue kitambaa kingine ushone mpya. Huo ndio mfano unaoakisi katiba ya Tanzania ambayo kimsingi haikidhi haja ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa sababu yenyewe asili yake ni katiba ya chama kimoja.

Pamoja na kupigania mabadiliko ya katiba, Profesa Haroub alikuwa mstari wa mbele kupigania kuwapo kwa Tume huru za uchaguzi ili kufanyika kwa chaguzi huru na haki hapa Tanzania. Kwa maneno mepesi ni kwamba alikuwa mwanademokrasia mtetezi wa wanyonge na mpiganaji wa haki za binadamu.

Kwa kuwa alikuwa muwazi na msema kweli, wapo viongozi ambao hawakumpenda na wako wengine walimnasibisha na chama cha siasa hasa cha upinzani, lakini kimsingi Profesa Haroub hakujifunga na chama chochote cha siasa na ndiyo maana akawa anaweza kukosoa na kusema kweli. Alichokuwa akikikosoa si chama bali ni mfumo wa siasa uliopo nchini na kwamba mfumo huo kubadilishika kwake ni lazima uanzie katika katiba.

Pamoja na usomi wote aliokuwa nao, Profesa Haroub hakujitenga na watu wa kawaida, alishiriki katika shughuli na hafla mbalimbali alizotaarifiwa. Mimi alinifanya kama mtani wake, alikuwa akiweza kunipigia simu na kunambia; “hivi sasa niko kwenu Pemba, vipi nikuletee mashelisheli?”
Profesa Haroub pamoja na usomi wake, alijichanganya!

Kitu kimoja muhimu nilichokigundua kwake ni kwamba pamoja na kuwa alikuwa tayari kushirikiana na vyombo vya habari kwa wakati wowote ule lakini alikuwa makini. Neno lake kila siku lilikuwa ‘nisikilize kwa makini, usininukuu vibaya.’

Pamoja na kwamba alikuwa na kazi nyingi, midahalo mingi na mihadhara mingi lakini utashangaa jinsi alivyokuwa na shauku ya kusoma. Ofisini kwake hakuingiliki, vitabu kila pembe, vimefurika mpaka vimepitiliza, lakini hakuwa akisahau alipoweka kitabu. Unapokwenda kufanya mahojiano naye na ukawa unataka kumrikodi ni lazima usogeze kidogo vitabu na makabrasha yatakayokuwapo mezani kwake au ukiweke kitonge (tape recorder) chako juu ya vitabu.

Siku moja nilibahatika kufika nyumbani kwake pale Chuo Kikuu, nako mambo hayakuwa tofauti sana na ofisini kwani mashubaka yote yalijaa vitabu, meza za ukumbini nazo zilikuwa na vitabu vilivyofunuliwa kuonyesha kuwa wapo watu waliokuwa wakifanya kazi ya kusoma na kuongeza ujuzi. Kwa bahati nzuri mke aliyemuoa ni sawa na yeye, Profesa Saida Yahya Othman, naye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, hivyo wote walikuwa ni wapenzi wa kusoma, wakawa wamefanana sawasawa kama sahani na kawa.

Kimaumbile Profesa Haroub alikuwa ni mpole lakini makini, hakuwa msemaji ovyo na alikuwa ni msikilizaji mzuri, na hiyo ndiyo sifa ya mtu anayependa kujifunza, hakuwa mtu mwenye dharau hata kidogo, hata kama ulichomuuliza sicho, atakujibu kwa hekima kubwa huku akikuelekeza kilicho ndicho, kwamba ‘tatizo si hilo bali ni kitu fulani na ambacho nadhani kimesababishwa na kitu fulani.’


Mwaka 1992 Profesa Haroub akishirikiana na wenzake, Fatma Maghimbi na Hassan Said walianzisha Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Zanzibar baada ya kuona kwamba jamii ya Kizanzibari inahitaji kufahamu haki zao na kuwa na taasisi ambayo angalau itasimamia kutendeka kwa haki.

Azma ya kituo hicho ambacho hadi umauti ulipomkuta, Profesa Haroub alikuwa mwenyekiti wake, ni kuhakikisha kuwa kila mkazi wa Zanzibar hususan masikini, wanawake, watoto, walemavu na makundi mengine yenye nafasi finyu katika jamii wanaelewa kuhusu haki zao za msingi na wanazifanyia kazi ili kujenga jamii inayofuata misingi ya sheria na inayoongozwa na utawala bora.

Siku moja nilizungumza na Profesa Haroub kuhusu uwepo wa kituo hicho na suala zima la utawala bora Zanzibar naye akasema; “ni vigumu kuwa na utawala bora ikiwa watu wanaoongozwa hawajui hata maana yake, hawaelewi umuhimu wa sheria na kwa ufupi hawajui haki zao. Hivyo dhamira kuu ya kuanzisha kituo hicho ni kuwashajiisha Wazanzibari kujua haki zao kwa kuwapa mafunzo kwa njia tofauti na pia kuwasaidia kutetea haki zao.

Nilipozungumza naye alinambia kuwa kituo hicho kimedhamiria kuinua upeo wa wananchi juu ya masuala ya sheria, haki na wajibu wa mwananchi kwa nchi yake kwa kuendesha semina, warsha, mikutano pamoja na kutoa ushauri wa kisheria.

Profesa Haroub hakuishia hapo bali alieleza pia uzoefu wake kwa watu wenye madaraka na alisema “kuna tabia ya watu hasa wenye mamlaka kuchezea sheria, wanahisi kama kwamba sheria haiwahusu au hata kama inamuhusu anaweza kuipinda, ikiwa watu kama hao wataendelea kupewa mwanya katika jamii, suala la utawala bora litakuwa ni la hadithini tu.

“Haitoshi kutamka kwamba unafuata utawala bora, au hata kuwa na Wizara inayoshughulikia masuala ya utawala bora, halafu wanaovunja haki za binadamu ni maafisa wa vyombo vya dola,” alisema Profesa Haroub.

Hayo ni baadhi tu ya matamshi yaliyotoka kwenye kinywa cha mwanadiplomasia, mwana demokrasia na mpiganaji wa haki za binadamu, Hayati Profesa Haroub Othman. Kifo chake kimeacha pengo kwa Watanzania wote, wanazuoni na wanajamii aliojitolea muda wake na uwezo wake kuwatetea, kuwafumbua macho, kuwazibua masikio na kuwaonyesha njia ya kuelekea kwenye utawala wa sheria na unaoheshimu haki za binadamu. Mchango wake kwa jamii ni mkubwa na bila shaka jitihada zake iko siku zitazaa matunda. Uliokufa ni mwili tu, fikra na mawazo yake bado yataendelea kuwapo. Profesa Haroub aliiaga dunia Juni 28, mjini Zanzibar na kuzikwa Juni 29, 2009.

Labels:

KUHUSU MIMI

JINA:Hawra Shamte
MAKAZI:Dar es salaam
NCHI:Tanzania
KAZI:Mwandishi

KUELEKEA BUNGE LA BAJETI 2006

QuickTopic free message boards
Bonyeza hapa ili uweze kuelezea: NINI MTAZAMO WAKO JUU YA BAJETI IJAYO YA MWAKA 2006/07 NCHINI TANZANIA?

VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI

  • The Citizen
  • Mwananchi
  • Mwanaspoti
  • Business Times
  • Majira
  • Daily News
  • Nipashe
  • The Guardian
  • The Express
  • Kiongozi
  • Uhuru/Mzalendo
  • Arusha Times
  • BLOGI ZA KISWAHILI

  • Bangaiza
  • Mwandani
  • Pambazuko
  • Damija
  • Mtafiti
  • Martha
  • Gaphiz
  • Swahili time
  • Miruko
  • Dira yangu
  • Msangimdogo
  • Jeff Msangi
  • Kasri la mwanazuoni
  • Kurunzi
  • Baragumu
  • Mawazohuru
  • Fikra Thabiti
  • Mtandaoni
  • Motowaka
  • Mkwinda
  • Ngurumo
  • Nyembo
  • Bwaya
  • Omega
  • Tafakari za Maisha
  • Nuru akilini
  • Mtandawazi
  • Mhujumu
  • Vijimamboz
  • Wakati wa Ukombozi
  • Kijiwe Joto
  • Watoto Wetu
  • Jungu kuu
  • Kisima cha Weledi
  • Jarida la Ughaibuni
  • Bhalezee
  • Sauti ya Baragumu
  • Kona yangu
  • Furahia Maisha
  • Bakanja
  • Terrie Swai
  • Fatma Karama
  • Kazonta
  • Binti Afrika
  • Blogu ya Kilimo
  • Ukombozi
  • Mwafrika
  • Digital Africa
  • Blogu ya lugha mseto
  • BLOGI ZA WAAFRIKA

  • BLOGAFRICA
  • BLOGU ZA WAAFRIKA
  • DIGITAL AFRICA
  • MAMA JUNKYARD'S
  • MSHAIRI
  • KENYAN PUNDIT
  • MONGI DREAMS
  • ISARIA MWENDE
  • CUNNING LINGUISTICA
  • ETHIOPUNDIT
  • MOCHALICIOUS
  • UNGANISHA
  • DEMOKRASIA KENYA
  • CHANUKA
  • BANKELE
  • MAARIFA/AKIEY
  • AFROMUSING
  • NEHANDA DREAMS
  • BLACK LOOKS
  • YUMMY WAKAME
  • AFRICAN OIL POLITICS
  • NUBIAN SOUL
  • SANAA
  • VIRTUAL INSANITY
  • MENTAL ACROBATICS
  • KENYA UNLIMITED
  • JIKUMBUSHE KAZI ZANGU ZA ZAMANI

    April 2006 May 2006 June 2006 October 2007 November 2007 December 2007 May 2008 July 2008 October 2008 July 2009 August 2012 October 2012

    Imetengenezwa na

    Ukibofya hapa utapelekwa katika Blogi ya msangimdogo

    na inawezeshwa na