" Jamii iliyostaarabika ni yenye kuheshimu Mawazo & Mitazamo ya wengine. Mchango wako katika kazi yoyote ulenge kujenga jamii yenye Kujitambua, Kujithamini na Kujiwajibisha "

 
Tuesday, July 14, 2009

 Fikra pevu kamwe haitakufa

NI vigumu kuamini, lakini ni kweli, wakati wake ulifika, aliitwa naye akaitika. Atakumbukwa kwa mengi mazuri, hasa kwa mchango wake kwa jamii. Mpiganaji wa haki za binadamu na msema kweli.

Profesa Haroub Othman Miraji (68) ni vigumu kwa anayemtambua kuamini kuwa ametutoka, amekwenda kwenye pumziko la milele. Ingawa binadamu hapendi kuamini linapomtokea linalomuhuzunisha, au kwa vile ana tabia ya kupenda kusikia yale yanayompendeza tu, kifo cha Profesa Haroub kilitufanya wengi kutoziruhusu akili zetu kukubali ukweli, lakini bado ukweli unabaki pale pale, kwamba pamoja na kuwa tulimhitaji lakini Mungu alimhitaji zaidi, wakati wake ulifika, aliitwa na akaitika.

Kama mpigania haki mashuhuri wa Afrika Kusini Steven Biko alivyowahi kusema kwamba ‘fikra njema ni ile isiyokufa na ni vema kufa kimwili kuliko kufa kifikra,’ fikra na mawazo ya Profesa Haroub yatadumu milele, ulioondoka kwetu ni mwili tu lakini fikra zake zitabaki kuwa hai kwa wanamapinduzi na wapigania haki za wanyonge.

Profesa Haroub ni alama ya fikra pevu, mahiri na yenye busara. Pamoja na wadhifa aliokuwa nao na heshima katika jamii lakini alikuwa mtu wa watu, tayari kuzungumza na kila aliyemkabili, hakubagua mdogo wala mkubwa, kwake yeye mwenye elimu na asiyekuwa na elimu hakuwa na tofauti katika misingi ya kibinadamu.

Aliamini kwa dhati kwamba binadamu wote ni sawa, hakujikweza wala hakutakabari. Binafsi Profesa Haroub alikuwa ni chanzo changu cha habari (source). Kila ninapotingwa na jambo hasa katika masuala ya siasa, mitafuruku na migogoro yake, Profesa Haroub ndiye aliyekuwa kimbilio langu, simu moja tu ilitosha kupanga naye miadi ya kufanya mahojiano na kama hayupo nchini atakwambia ‘niandikie maswali unitumie mtandaoni.’ Ukimwambia muda wa mwisho wa kuwasilisha, hakikisha kwamba majibu yako utayapata ndani ya muda mulioahidiana. Ukimwambia nitakuja ofisini kwako saa tatu asubuhi, saa tatu kasoro robo yeye atakuwa ameshafika.

Profesa Haroub alikuwa mahiri katika kudadavua suala la kisiasa Zanzibar na pia alikuwa rejea muhimu katika masuala ya katiba na sheria. Bila kigugumizi Profesa Haroub siku moja aliniambia kwamba ‘Katiba ya Tanzania imejaa viraka,’ nami nikaandika hivyo katika makala. Hata hivyo hakuishia hapo ila alivieleza viraka vingi vilivyomo katika katiba na kisha kutoa ushauri. Alisema kwamba kama nguo imejaa viraka kweli yaweza kuvalika? Uking’ang’ania kuivaa bila shaka siku moja itakuadhiri. Akaendelea kusema kwamba nguo yenye viraka vingi inapoteza uhalisia wake, inapoteza taswira yake ya awali, hivyo kama uliupenda mshono wake ni vema ununue kitambaa kingine ushone mpya. Huo ndio mfano unaoakisi katiba ya Tanzania ambayo kimsingi haikidhi haja ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa sababu yenyewe asili yake ni katiba ya chama kimoja.

Pamoja na kupigania mabadiliko ya katiba, Profesa Haroub alikuwa mstari wa mbele kupigania kuwapo kwa Tume huru za uchaguzi ili kufanyika kwa chaguzi huru na haki hapa Tanzania. Kwa maneno mepesi ni kwamba alikuwa mwanademokrasia mtetezi wa wanyonge na mpiganaji wa haki za binadamu.

Kwa kuwa alikuwa muwazi na msema kweli, wapo viongozi ambao hawakumpenda na wako wengine walimnasibisha na chama cha siasa hasa cha upinzani, lakini kimsingi Profesa Haroub hakujifunga na chama chochote cha siasa na ndiyo maana akawa anaweza kukosoa na kusema kweli. Alichokuwa akikikosoa si chama bali ni mfumo wa siasa uliopo nchini na kwamba mfumo huo kubadilishika kwake ni lazima uanzie katika katiba.

Pamoja na usomi wote aliokuwa nao, Profesa Haroub hakujitenga na watu wa kawaida, alishiriki katika shughuli na hafla mbalimbali alizotaarifiwa. Mimi alinifanya kama mtani wake, alikuwa akiweza kunipigia simu na kunambia; “hivi sasa niko kwenu Pemba, vipi nikuletee mashelisheli?”
Profesa Haroub pamoja na usomi wake, alijichanganya!

Kitu kimoja muhimu nilichokigundua kwake ni kwamba pamoja na kuwa alikuwa tayari kushirikiana na vyombo vya habari kwa wakati wowote ule lakini alikuwa makini. Neno lake kila siku lilikuwa ‘nisikilize kwa makini, usininukuu vibaya.’

Pamoja na kwamba alikuwa na kazi nyingi, midahalo mingi na mihadhara mingi lakini utashangaa jinsi alivyokuwa na shauku ya kusoma. Ofisini kwake hakuingiliki, vitabu kila pembe, vimefurika mpaka vimepitiliza, lakini hakuwa akisahau alipoweka kitabu. Unapokwenda kufanya mahojiano naye na ukawa unataka kumrikodi ni lazima usogeze kidogo vitabu na makabrasha yatakayokuwapo mezani kwake au ukiweke kitonge (tape recorder) chako juu ya vitabu.

Siku moja nilibahatika kufika nyumbani kwake pale Chuo Kikuu, nako mambo hayakuwa tofauti sana na ofisini kwani mashubaka yote yalijaa vitabu, meza za ukumbini nazo zilikuwa na vitabu vilivyofunuliwa kuonyesha kuwa wapo watu waliokuwa wakifanya kazi ya kusoma na kuongeza ujuzi. Kwa bahati nzuri mke aliyemuoa ni sawa na yeye, Profesa Saida Yahya Othman, naye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, hivyo wote walikuwa ni wapenzi wa kusoma, wakawa wamefanana sawasawa kama sahani na kawa.

Kimaumbile Profesa Haroub alikuwa ni mpole lakini makini, hakuwa msemaji ovyo na alikuwa ni msikilizaji mzuri, na hiyo ndiyo sifa ya mtu anayependa kujifunza, hakuwa mtu mwenye dharau hata kidogo, hata kama ulichomuuliza sicho, atakujibu kwa hekima kubwa huku akikuelekeza kilicho ndicho, kwamba ‘tatizo si hilo bali ni kitu fulani na ambacho nadhani kimesababishwa na kitu fulani.’


Mwaka 1992 Profesa Haroub akishirikiana na wenzake, Fatma Maghimbi na Hassan Said walianzisha Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Zanzibar baada ya kuona kwamba jamii ya Kizanzibari inahitaji kufahamu haki zao na kuwa na taasisi ambayo angalau itasimamia kutendeka kwa haki.

Azma ya kituo hicho ambacho hadi umauti ulipomkuta, Profesa Haroub alikuwa mwenyekiti wake, ni kuhakikisha kuwa kila mkazi wa Zanzibar hususan masikini, wanawake, watoto, walemavu na makundi mengine yenye nafasi finyu katika jamii wanaelewa kuhusu haki zao za msingi na wanazifanyia kazi ili kujenga jamii inayofuata misingi ya sheria na inayoongozwa na utawala bora.

Siku moja nilizungumza na Profesa Haroub kuhusu uwepo wa kituo hicho na suala zima la utawala bora Zanzibar naye akasema; “ni vigumu kuwa na utawala bora ikiwa watu wanaoongozwa hawajui hata maana yake, hawaelewi umuhimu wa sheria na kwa ufupi hawajui haki zao. Hivyo dhamira kuu ya kuanzisha kituo hicho ni kuwashajiisha Wazanzibari kujua haki zao kwa kuwapa mafunzo kwa njia tofauti na pia kuwasaidia kutetea haki zao.

Nilipozungumza naye alinambia kuwa kituo hicho kimedhamiria kuinua upeo wa wananchi juu ya masuala ya sheria, haki na wajibu wa mwananchi kwa nchi yake kwa kuendesha semina, warsha, mikutano pamoja na kutoa ushauri wa kisheria.

Profesa Haroub hakuishia hapo bali alieleza pia uzoefu wake kwa watu wenye madaraka na alisema “kuna tabia ya watu hasa wenye mamlaka kuchezea sheria, wanahisi kama kwamba sheria haiwahusu au hata kama inamuhusu anaweza kuipinda, ikiwa watu kama hao wataendelea kupewa mwanya katika jamii, suala la utawala bora litakuwa ni la hadithini tu.

“Haitoshi kutamka kwamba unafuata utawala bora, au hata kuwa na Wizara inayoshughulikia masuala ya utawala bora, halafu wanaovunja haki za binadamu ni maafisa wa vyombo vya dola,” alisema Profesa Haroub.

Hayo ni baadhi tu ya matamshi yaliyotoka kwenye kinywa cha mwanadiplomasia, mwana demokrasia na mpiganaji wa haki za binadamu, Hayati Profesa Haroub Othman. Kifo chake kimeacha pengo kwa Watanzania wote, wanazuoni na wanajamii aliojitolea muda wake na uwezo wake kuwatetea, kuwafumbua macho, kuwazibua masikio na kuwaonyesha njia ya kuelekea kwenye utawala wa sheria na unaoheshimu haki za binadamu. Mchango wake kwa jamii ni mkubwa na bila shaka jitihada zake iko siku zitazaa matunda. Uliokufa ni mwili tu, fikra na mawazo yake bado yataendelea kuwapo. Profesa Haroub aliiaga dunia Juni 28, mjini Zanzibar na kuzikwa Juni 29, 2009.

Labels:

1 Maoni ya Wasomaji:

Anonymous Obat pelangsing alami anasema...

Nice blog and article, thanks for sharing. Meizitang Botanical

12:15 PM  

Post a Comment

<< Rudi mwanzo

KUHUSU MIMI

JINA:Hawra Shamte
MAKAZI:Dar es salaam
NCHI:Tanzania
KAZI:Mwandishi

KUELEKEA BUNGE LA BAJETI 2006

QuickTopic free message boards
Bonyeza hapa ili uweze kuelezea: NINI MTAZAMO WAKO JUU YA BAJETI IJAYO YA MWAKA 2006/07 NCHINI TANZANIA?

VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI

  • The Citizen
  • Mwananchi
  • Mwanaspoti
  • Business Times
  • Majira
  • Daily News
  • Nipashe
  • The Guardian
  • The Express
  • Kiongozi
  • Uhuru/Mzalendo
  • Arusha Times
  • BLOGI ZA KISWAHILI

  • Bangaiza
  • Mwandani
  • Pambazuko
  • Damija
  • Mtafiti
  • Martha
  • Gaphiz
  • Swahili time
  • Miruko
  • Dira yangu
  • Msangimdogo
  • Jeff Msangi
  • Kasri la mwanazuoni
  • Kurunzi
  • Baragumu
  • Mawazohuru
  • Fikra Thabiti
  • Mtandaoni
  • Motowaka
  • Mkwinda
  • Ngurumo
  • Nyembo
  • Bwaya
  • Omega
  • Tafakari za Maisha
  • Nuru akilini
  • Mtandawazi
  • Mhujumu
  • Vijimamboz
  • Wakati wa Ukombozi
  • Kijiwe Joto
  • Watoto Wetu
  • Jungu kuu
  • Kisima cha Weledi
  • Jarida la Ughaibuni
  • Bhalezee
  • Sauti ya Baragumu
  • Kona yangu
  • Furahia Maisha
  • Bakanja
  • Terrie Swai
  • Fatma Karama
  • Kazonta
  • Binti Afrika
  • Blogu ya Kilimo
  • Ukombozi
  • Mwafrika
  • Digital Africa
  • Blogu ya lugha mseto
  • BLOGI ZA WAAFRIKA

  • BLOGAFRICA
  • BLOGU ZA WAAFRIKA
  • DIGITAL AFRICA
  • MAMA JUNKYARD'S
  • MSHAIRI
  • KENYAN PUNDIT
  • MONGI DREAMS
  • ISARIA MWENDE
  • CUNNING LINGUISTICA
  • ETHIOPUNDIT
  • MOCHALICIOUS
  • UNGANISHA
  • DEMOKRASIA KENYA
  • CHANUKA
  • BANKELE
  • MAARIFA/AKIEY
  • AFROMUSING
  • NEHANDA DREAMS
  • BLACK LOOKS
  • YUMMY WAKAME
  • AFRICAN OIL POLITICS
  • NUBIAN SOUL
  • SANAA
  • VIRTUAL INSANITY
  • MENTAL ACROBATICS
  • KENYA UNLIMITED
  • JIKUMBUSHE KAZI ZANGU ZA ZAMANI

    April 2006 May 2006 June 2006 October 2007 November 2007 December 2007 May 2008 July 2008 October 2008 July 2009 August 2012 October 2012

    Imetengenezwa na

    Ukibofya hapa utapelekwa katika Blogi ya msangimdogo

    na inawezeshwa na