Je taifa lisilo na miiko, sera wala dira ni taifa hai?
Na Hawra Shamte
KUNA watu ambao wamejaaliwa, wamejaaliwa vipawa na maono, au labda niseme wana fikra pevu, fikra zao hufanya kazi katika zama tofauti tofauti.
Watu hao wana uwezo mkubwa wa kufikiri, kutafakuri na hata kuyajadili mambo, wana uwezo wa kudadavua. Hao ndio wanaoitwa ‘wanafalsafa’ hawa ni kama akina Machiavelli, John Stuart Mill, W. Rostow na wengineo wengi kutoka katika dunia iliyoendelea.
Lakini kwa bahati hata katika ulimwengu wa tatu, wako watu ‘vichwa’ wenye uwezo mkubwa wa kufikiri na katika orodha ya watu hao, baba wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere ni mmoja wao. Fikra zake bado ziko hai kama alivyosema Steven Bhiko, mwanaharakati wa kupigania haki za weusi wa Afrika Kusini katika miaka ya 60. Bhiko alisema ni bora kuwa na fikra hai kuliko fikra mfu kwani ni bora kiwiliwili kinachokufa kuliko fikira iliyokufa.
Angalau twaweza kusema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi iliyojaaliwa kuwa na watu wenye fikra hai, mmoja wapo ni hayati Mwalimu Julius Nyerere. Kilichokufa ni kiwiliwili tu, fikra na busara zake bado zipo na zitadumu milele kwani vitabu vya historia vitawakumbusha wanadamu zama hadi zama.
Watanzania tukipata nafasi tuzichambue na tuzitafakari fikira mbalimbali za Mwalimu Nyerere. Mwalimu Nyerere alikuwa muwazi na mkweli, alikemea rushwa na ufisadi kwa dhati na alisema kuwa kiongozi ni lazima aonyeshe kuichukia rushwa kwa dhati, kinyume cha hivyo huyo si kiongozi anayeifaa Tanzania.
Inasikitisha sana leo hii, kuona viongozi wakiwatetea wala rushwa, wakikemea rushwa midomoni wakati maneno yao hayaonyeshi taathira yake katika vitendo. Zama za Mwalimu Nyerere na Edward Moringe Sokoine tuliwaona wahujumu uchumi jinsi walivyoadhirika. Waliopenda kujilimbikizia mali walifanya hivyo kwa tahadhari kubwa, kwani wakigundulika, taadhira uwanjani.
Leo hii viongozi wanaona fahari kuwa na mali isiyohesabika wala kutajika, wanaona raha kuambiwa kwamba wao ni matajiri/mabepari, na baya zaidi hakuna hata anayethubutu kuwanyooshea vidole au angalau kuwauliza mali hii mumeipata wapi. Watu wanaishi raha mustarehe wala nadhari haziwasuti kwamba kuna wenzao wanaoshinda na kulalia kipande cha muhogo wa kuchemsha kwani hata kile kipande cha nguru cha hela tano hakipatikani tena.
Wakati Mwalimu alipoweka miiko na maadili ya uongozi aliona mbali, na hilo alilizungumza hadharani kwamba taifa lisilo na miiko na maadili ni taifa mfu. Haiwezekani binadamu kumwachia uhuru usio na mipaka, awe na uhuru wa kuamua, awe na uhuru wa kuchukua na awe na uhuru wa kung’ang’ania na hata kuiba. Ni lazima uhuru uwe na mipaka, kwamba tunakupa dhamana ya kuongoza lakini ni mwiko kumiliki mali, ni mwiko kuwa na nyumba za kupangisha, ni mwiko kuwa na mishahara miwili, ni mwiko…
Ingawa yawezekana katika zama hizi za ujasiriamali miiko hiyo imepitwa na wakati, sasa viongozi wetu wanaruhusiwa kufanya biashara na kuwa na mitaji mikubwa mikubwa, lakini je ni wapi tunapiga mstari baina ya mali ya umma na mali ya kiongozi binafsi? Ni vipi tunamzuia kuchota katika hazina ya taifa? Au ni vipi tunamdhibiti asiingie mikataba inayonuka rushwa? Hili ni vigumu kulidhibiti kama hakuna miiko inayoeleweka.
Uongozi usiokuwa na miiko si uongozi wa kidemokrasia, huo ni utawala wa kifalme na ndiyo maana leo hii tunashuhudia familia zinaingia katika safu za uongozi. Baba ni kiongozi wa ngazi fulani, mama ni kiongozi wa ngazi ya chini yake na hata watoto nao wanakimbilia kupanda ngazi za uongozi. Hali hii tukiiruhusu kuna siku tutajikuta tumejenga himaya ya kifalme, badala ya kwenda mbele, tunarudi nyuma.
Hakuna miiko, hakuna dira wala mwelekeo, mwenye nguvu mpishe. Tuliambiwa ukimuona mtu anakimbilia madaraka muogope, kwani madaraka ni dhamana nzito isiyopaswa kukimbiliwa, kwani jamani ‘Ikulu’ kuna biashara gani? Katika mantiki haya Ikulu yaweza tu kuwa ni nembo ya uongozi, lakini kukimbilia madaraka katika ngazi yoyote ya uongozi ni jambo lisiloingia akilini kwa mtu anayefahamu uzito wa madaraka, ni sawa na mzigo mzito anaotwisha mtu kichwani kwake ambao huchosha mabega yake na hata miguu yake, akiutua hushukuru, kwani huwa ametolewa mbali!
Kiongozi anapaswa akose amani watu wake wanapolala njaa, kichwa kimzunguke anaposikia mashakil yanayowakabili watu wake, akose usingizi kwa kufikiria jinsi ya kutatua matatizo ya watu wake? Wakati wenzake wanakaa vitini, yeye kiti hakimuweki, lazima azunguke ofisi na kukuna kichwa. Yote haya si mambo ya kuyakimbilia kwa mtu anayefahamu uzito wa dhamana ya uongozi.
Angalia Tanzania yetu ya leo jinsi watu wanavyolilia kupata uongozi wa umma kwa njia yoyote ile, wako tayari kutoa vyao, ikibidi vyote kwa imani ya kuwa miaka mitano ya uongozi atavirudisha na ziada atapata. Huo kwa kweli si uongozi wa umma, Watanzania tunapaswa twende tukaichote ile hazina ya busara aliyotuachia baba wa taifa.
Tukisema tunajiuliza wapi tunapokosea, tutajikuta hatujawahi kupatia kitu, sasa na tujiulize ni njia ipi sahihi ya kuifuata? Je taifa lisilo na dira na mwelekeo ni taifa hai?
Hawra Shamte ni Mhariri wa Siasa wa Gazeti la Mwananchi.
hshamte@mwananchi.co.tz
0754 849694