" Jamii iliyostaarabika ni yenye kuheshimu Mawazo & Mitazamo ya wengine. Mchango wako katika kazi yoyote ulenge kujenga jamii yenye Kujitambua, Kujithamini na Kujiwajibisha "

 
Thursday, October 25, 2007

 Je taifa lisilo na miiko, sera wala dira ni taifa hai?

Na Hawra Shamte

KUNA watu ambao wamejaaliwa, wamejaaliwa vipawa na maono, au labda niseme wana fikra pevu, fikra zao hufanya kazi katika zama tofauti tofauti.

Watu hao wana uwezo mkubwa wa kufikiri, kutafakuri na hata kuyajadili mambo, wana uwezo wa kudadavua. Hao ndio wanaoitwa ‘wanafalsafa’ hawa ni kama akina Machiavelli, John Stuart Mill, W. Rostow na wengineo wengi kutoka katika dunia iliyoendelea.

Lakini kwa bahati hata katika ulimwengu wa tatu, wako watu ‘vichwa’ wenye uwezo mkubwa wa kufikiri na katika orodha ya watu hao, baba wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere ni mmoja wao. Fikra zake bado ziko hai kama alivyosema Steven Bhiko, mwanaharakati wa kupigania haki za weusi wa Afrika Kusini katika miaka ya 60. Bhiko alisema ni bora kuwa na fikra hai kuliko fikra mfu kwani ni bora kiwiliwili kinachokufa kuliko fikira iliyokufa.

Angalau twaweza kusema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi iliyojaaliwa kuwa na watu wenye fikra hai, mmoja wapo ni hayati Mwalimu Julius Nyerere. Kilichokufa ni kiwiliwili tu, fikra na busara zake bado zipo na zitadumu milele kwani vitabu vya historia vitawakumbusha wanadamu zama hadi zama.

Watanzania tukipata nafasi tuzichambue na tuzitafakari fikira mbalimbali za Mwalimu Nyerere. Mwalimu Nyerere alikuwa muwazi na mkweli, alikemea rushwa na ufisadi kwa dhati na alisema kuwa kiongozi ni lazima aonyeshe kuichukia rushwa kwa dhati, kinyume cha hivyo huyo si kiongozi anayeifaa Tanzania.

Inasikitisha sana leo hii, kuona viongozi wakiwatetea wala rushwa, wakikemea rushwa midomoni wakati maneno yao hayaonyeshi taathira yake katika vitendo. Zama za Mwalimu Nyerere na Edward Moringe Sokoine tuliwaona wahujumu uchumi jinsi walivyoadhirika. Waliopenda kujilimbikizia mali walifanya hivyo kwa tahadhari kubwa, kwani wakigundulika, taadhira uwanjani.

Leo hii viongozi wanaona fahari kuwa na mali isiyohesabika wala kutajika, wanaona raha kuambiwa kwamba wao ni matajiri/mabepari, na baya zaidi hakuna hata anayethubutu kuwanyooshea vidole au angalau kuwauliza mali hii mumeipata wapi. Watu wanaishi raha mustarehe wala nadhari haziwasuti kwamba kuna wenzao wanaoshinda na kulalia kipande cha muhogo wa kuchemsha kwani hata kile kipande cha nguru cha hela tano hakipatikani tena.

Wakati Mwalimu alipoweka miiko na maadili ya uongozi aliona mbali, na hilo alilizungumza hadharani kwamba taifa lisilo na miiko na maadili ni taifa mfu. Haiwezekani binadamu kumwachia uhuru usio na mipaka, awe na uhuru wa kuamua, awe na uhuru wa kuchukua na awe na uhuru wa kung’ang’ania na hata kuiba. Ni lazima uhuru uwe na mipaka, kwamba tunakupa dhamana ya kuongoza lakini ni mwiko kumiliki mali, ni mwiko kuwa na nyumba za kupangisha, ni mwiko kuwa na mishahara miwili, ni mwiko…

Ingawa yawezekana katika zama hizi za ujasiriamali miiko hiyo imepitwa na wakati, sasa viongozi wetu wanaruhusiwa kufanya biashara na kuwa na mitaji mikubwa mikubwa, lakini je ni wapi tunapiga mstari baina ya mali ya umma na mali ya kiongozi binafsi? Ni vipi tunamzuia kuchota katika hazina ya taifa? Au ni vipi tunamdhibiti asiingie mikataba inayonuka rushwa? Hili ni vigumu kulidhibiti kama hakuna miiko inayoeleweka.

Uongozi usiokuwa na miiko si uongozi wa kidemokrasia, huo ni utawala wa kifalme na ndiyo maana leo hii tunashuhudia familia zinaingia katika safu za uongozi. Baba ni kiongozi wa ngazi fulani, mama ni kiongozi wa ngazi ya chini yake na hata watoto nao wanakimbilia kupanda ngazi za uongozi. Hali hii tukiiruhusu kuna siku tutajikuta tumejenga himaya ya kifalme, badala ya kwenda mbele, tunarudi nyuma.

Hakuna miiko, hakuna dira wala mwelekeo, mwenye nguvu mpishe. Tuliambiwa ukimuona mtu anakimbilia madaraka muogope, kwani madaraka ni dhamana nzito isiyopaswa kukimbiliwa, kwani jamani ‘Ikulu’ kuna biashara gani? Katika mantiki haya Ikulu yaweza tu kuwa ni nembo ya uongozi, lakini kukimbilia madaraka katika ngazi yoyote ya uongozi ni jambo lisiloingia akilini kwa mtu anayefahamu uzito wa madaraka, ni sawa na mzigo mzito anaotwisha mtu kichwani kwake ambao huchosha mabega yake na hata miguu yake, akiutua hushukuru, kwani huwa ametolewa mbali!

Kiongozi anapaswa akose amani watu wake wanapolala njaa, kichwa kimzunguke anaposikia mashakil yanayowakabili watu wake, akose usingizi kwa kufikiria jinsi ya kutatua matatizo ya watu wake? Wakati wenzake wanakaa vitini, yeye kiti hakimuweki, lazima azunguke ofisi na kukuna kichwa. Yote haya si mambo ya kuyakimbilia kwa mtu anayefahamu uzito wa dhamana ya uongozi.

Angalia Tanzania yetu ya leo jinsi watu wanavyolilia kupata uongozi wa umma kwa njia yoyote ile, wako tayari kutoa vyao, ikibidi vyote kwa imani ya kuwa miaka mitano ya uongozi atavirudisha na ziada atapata. Huo kwa kweli si uongozi wa umma, Watanzania tunapaswa twende tukaichote ile hazina ya busara aliyotuachia baba wa taifa.

Tukisema tunajiuliza wapi tunapokosea, tutajikuta hatujawahi kupatia kitu, sasa na tujiulize ni njia ipi sahihi ya kuifuata? Je taifa lisilo na dira na mwelekeo ni taifa hai?

Hawra Shamte ni Mhariri wa Siasa wa Gazeti la Mwananchi.
hshamte@mwananchi.co.tz
0754 849694

Tuesday, October 09, 2007

 Kama Rais haelewi, nasi pia hatuelewi

Rais haelewi kwanini Tanzania bado ni masikini, nasi pia hatuelewi
Na Hawra Shamte

RAIS Jakaya Kikwete wiki iliyopita alipokuwa nchini Ufaransa aliulizwa na waandishi wa habari kwanini Tanzania inashindwa kujinasua kutoka katika lindi la umasikini? Rais alijibu kwa kweli hata yeye haelewi ni kwanini?

Rais anayo haki ya kujibu hivyo alivyojibu kwa sababu ni vigumu kuidadavua sababu hasa inayopelekea Tanzania iendelee kuwa masikini.

Tanzania ni nchi iliyobarikiwa utajiri na rasilimali za kila aina, mito itiririshayo maji, maziwa yanayosaidia katika uzalishaji wa umeme, bahari yenye samaki an-wai, milima, mabonde yenye rutuba ya kilimo, ardhi yenye madini, almasi, dhahabu, uranium, tanzanite, ruby na kadhalika. Misitu yenye wanyama wa kila aina, pamoja na yote hayo Tanzania imejaaliwa kuwa na hali ya hewa nzuri.

Tanzania imebahatika si miongoni mwa nchi zinazopata majanga ya asili mara kwa mara. Kwa kuwa Tanzania iko chini ya mstari wa Ikweta hivyo ni nchi yenye joto, lakini joto lake si la kutisha, kuna maeneo nchini ambayo katika kipindi kirefu hupata baridi lakini pia baridi yake si ya hatari. Hivyo hali ya hewa ya Tanzania ni ya wastani. Kwa kweli Tanzania imebarikiwa, sasa kwanini ni miongoni mwa nchi maskini sana duniani?

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne, watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Tanzania ina watu zaidi ya milioni 36, hivyo haina tatizo la watu. Tanzania ina ardhi yenye kilomita za mraba 945,000 hivyo haina uhaba wa ardhi, tena sehemu kubwa ya ardhi hiyo ina rutuba, katika hizo kilomita za mraba 62,000 ni maeneo yenye maji. Hivyo katika orodha ya Mwalimu Nyerere kumesalia vitu viwili, ambayo ni siasa safi na uongozi bora.

Je Tanzania tunayo siasa safi? Wakati wa zama za Ujamaa na Kujitegemea, Tanzania ilieleweka itikadi yake, hivyo hata siasa zake zilikuwa zina mrengo unaoeleweka. Katika zama hizi za utandawazi, Tanzania haina tena mwelekeo, haina dira, haina siasa inayoisimamia, haieleweki kama ni nchi ya kiliberali au ya kijamaa. Tanzania imekuwa bendera inafuata mvumo. Mvumo uliopo sasa ni soko huria, nayo ikafungua milango yake ya soko, lakini kwa bahati mbaya Tanzania haijaweza kuifungua milango ya masoko ya nchi tajiri ili nako iende ikapeleke bidhaa zake huko. Kwa ufupi suala la ‘siasa safi’ ni suala linalohitaji tafakuri pana. Je Tanzania inafuata siasa gani? Je hiyo siasa iliyopo ni safi?

Suala la uongozi bora ndilo linalotia kizunguzungu zaidi. Hapa hatupaswi kuwajadili watu bali kuijadili dhana nzima ya ‘uongozi,’ twapaswa tudadavue sifa za uongozi, je uongozi bora ni upi au uwe vipi? Bila shaka viko vigezo tunavyoweza kuvitumia ambavyo ni uwazi, ukweli, uwajibikaji, uadilifu, busara na demokrasia. Pengine viko vingi zaidi ya hivyo nilivyovitaja, lakini je uongozi wetu umezingatia vigezo hivyo? Hilo ni swali la kujiuliza.

Pengine hayo kwa kiasi fulani yanaweza kujibu lile swali la kwanini Tanzania ni masikini. Lakini pia iko dhana nyingine inayoelezwa na wasomi, kwamba Tanzania ni masikini kwa sababu Watanzania ni wavivu wa kufikiri. Hilo mimi siwezi kulipa udadavuzi wa kina, lakini akina Profesa Mwesiga Baregu, Issa Shivji na wengineo watakuwa wanao uchambuzi mzuri kuhusu hilo.

Lakini je, viongozi wetu wanapoingia mikataba mibovu huku dhamira zao zikiwa kwenye asilimia 10 (10%) bila kuzingatia maslahi ya taifa kwanza, je vipi tafakuri zao huwa kwa wakati huo?

Wakati tunapowakaribisha wahamishaji na tunawaita wawekezaji, huwa tunafikiri nini? Na wakati tunapofungua milango wazi ili mitandao ya wizi iingie, nini azma yetu inakuwa?

Wakati Rais alipoamua kuunda Baraza la Mawaziri lenye wajumbe 61, sijui kama alifikiria kama walipa kodi wa Tanzania wataumia kuubeba mzigo wa gharama kubwa za uendeshaji Serikali.

Wakati viongozi wanapokwenda ziarani nchi za nje kuomba msaada wa dola milioni 400 mathalan na kisha wakafuatana na ujumbe mkubwa ambao utatumia dola milioni 200 kuugharamia, je serikali huwa imefikiria nini?

Wanapojitokeza watu wakataka kuingia madarakani kwa udi na uvumba, hadi ikabidi wanunue Wapigakura, je dhamira yao hawa huwa ni nini? Je fikra zao zinakuwa pevu au mbichi?

Wakati kiongozi anapotamka kuwa ni lazima ndege inunuliwe hata kama ni mbovu na hata ikibidi wananchi wale majani, je mawazoni mwake huwa anachora taswira gani?

Wakati fedha za walipa kodi zinapotumiwa kwa kuwapa posho viongozi kuzunguka mikoani na wilayani kuelezea umuhimu wa bajeti, wanataka kutueleza nini? Je kama wao hawafikiri wanadhani wananchi wanaowaongoza hawana uwezo wa kufikiri pia?

Wakati anaposimamishwa ubunge, mbunge wa upinzani kwa sababu tu ya kutaka iundwe kamati huru ya Bunge kuchunguza mkataba wenye utata na Spika akasema kwa furaha kuwa “sauti ya Kigoma Kaskazini sasa haitasikika,” alikuwa akifiria nini?

Wakati tunapotoa maagizo ya kujenga shule bila kuongeza idadi ya walimu tunatarajia nini? Na wakati tunapotaka kutimiza mahitaji hayo ya walimu tuliyonayo kwa kuanzisha kozi za ualimu za miezi mitatu, je, huwa tunafikiri matokeo yake ya baadaye?

Tanzania imeshindwa kuendelea kwa miaka zaidi ya 46 tokea ijitawale, labda tunapaswa kuangalia mbali zaidi, tuangalie vikwazo vinavyotukabili vya nje na vya ndani. Je ni Watanzania tu ndio wavivu wa kufikiri au ni muundo wa mfumo wa dunia ulivyo?

Tumkumbuke mtaalam wa siasa-uchumi W.W.Rostow na hatua zake za ukuaji wa uchumi sambamba na mzunguko wa umasikini (visual circle of poverty). Walter Rodney naye aliandika ‘Vipi Ulaya imeifanya Afrika isiendelee’ labda tunapojiuliza kwanini bado tu masikini, Rostow na Rodney wanaweza kutupa jibu.

hshamte@mwananchi.co.tz
0754849694

KUHUSU MIMI

JINA:Hawra Shamte
MAKAZI:Dar es salaam
NCHI:Tanzania
KAZI:Mwandishi

KUELEKEA BUNGE LA BAJETI 2006

QuickTopic free message boards
Bonyeza hapa ili uweze kuelezea: NINI MTAZAMO WAKO JUU YA BAJETI IJAYO YA MWAKA 2006/07 NCHINI TANZANIA?

VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI

 • The Citizen
 • Mwananchi
 • Mwanaspoti
 • Business Times
 • Majira
 • Daily News
 • Nipashe
 • The Guardian
 • The Express
 • Kiongozi
 • Uhuru/Mzalendo
 • Arusha Times
 • BLOGI ZA KISWAHILI

 • Bangaiza
 • Mwandani
 • Pambazuko
 • Damija
 • Mtafiti
 • Martha
 • Gaphiz
 • Swahili time
 • Miruko
 • Dira yangu
 • Msangimdogo
 • Jeff Msangi
 • Kasri la mwanazuoni
 • Kurunzi
 • Baragumu
 • Mawazohuru
 • Fikra Thabiti
 • Mtandaoni
 • Motowaka
 • Mkwinda
 • Ngurumo
 • Nyembo
 • Bwaya
 • Omega
 • Tafakari za Maisha
 • Nuru akilini
 • Mtandawazi
 • Mhujumu
 • Vijimamboz
 • Wakati wa Ukombozi
 • Kijiwe Joto
 • Watoto Wetu
 • Jungu kuu
 • Kisima cha Weledi
 • Jarida la Ughaibuni
 • Bhalezee
 • Sauti ya Baragumu
 • Kona yangu
 • Furahia Maisha
 • Bakanja
 • Terrie Swai
 • Fatma Karama
 • Kazonta
 • Binti Afrika
 • Blogu ya Kilimo
 • Ukombozi
 • Mwafrika
 • Digital Africa
 • Blogu ya lugha mseto
 • BLOGI ZA WAAFRIKA

 • BLOGAFRICA
 • BLOGU ZA WAAFRIKA
 • DIGITAL AFRICA
 • MAMA JUNKYARD'S
 • MSHAIRI
 • KENYAN PUNDIT
 • MONGI DREAMS
 • ISARIA MWENDE
 • CUNNING LINGUISTICA
 • ETHIOPUNDIT
 • MOCHALICIOUS
 • UNGANISHA
 • DEMOKRASIA KENYA
 • CHANUKA
 • BANKELE
 • MAARIFA/AKIEY
 • AFROMUSING
 • NEHANDA DREAMS
 • BLACK LOOKS
 • YUMMY WAKAME
 • AFRICAN OIL POLITICS
 • NUBIAN SOUL
 • SANAA
 • VIRTUAL INSANITY
 • MENTAL ACROBATICS
 • KENYA UNLIMITED
 • JIKUMBUSHE KAZI ZANGU ZA ZAMANI

  April 2006 May 2006 June 2006 October 2007 November 2007 December 2007 May 2008 July 2008 October 2008 July 2009 August 2012 October 2012

  Imetengenezwa na

  Ukibofya hapa utapelekwa katika Blogi ya msangimdogo

  na inawezeshwa na