" Jamii iliyostaarabika ni yenye kuheshimu Mawazo & Mitazamo ya wengine. Mchango wako katika kazi yoyote ulenge kujenga jamii yenye Kujitambua, Kujithamini na Kujiwajibisha "

 
Thursday, May 01, 2008

 Haya ni mapambano ambayo wapenda demokrasia na amani lazima washinde!

Salaam
Makala hii ilitoka katika gazeti la Mwananchi la April 16, nimeona niiweke mtandaoni tufaidike wengi.

Kufuatia makubaliano ya mwafaka wa kisiasa Zanzibar kugota, baada ya Halmashauri Kuu ya CCM kuagiza kwamba suala la kuwapo kwa serikali shirikishi Zanzibar lirudishwe kwa wananchi kwa kupigiwa kura ya maoni, wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanaona kwamba, uamuzi huo unaweza kuzidisha utata wa kisiasa Zanzibar. Katika makala hii, mwandishi HAWRA SHAMTE anazungumza na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na haki za binadamu ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa HAROUB OTHMAN ambaye pamoja na mambo mengine anashauri kuwa viongozi wanapaswa kuhakikisha kwamba ufumbuzi wa tatizo la kisiasa Zanzibar unapatikana kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010…

Swali: Je, uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM kulirudisha suala la ‘Mwafaka’ kwa wananchi hasa kipengele cha serikali ya mseto, wewe unauonaje? Je, unaweza kuleta suluhisho la mgogoro?

JIBU: Ni jambo la busara kwa serikali kutaka wananchi wake watoe maoni/mapendekezo juu ya mambo yoyote makubwa au madogo inayotaka kufanya. Kuna nchi kama Switzerland ambapo serikali zake za mikoa (cantons) huitisha kura za maoni hata katika mambo madogo madogo. Huo ndio utamaduni waliokua nao. Sisi hapa hatuna utamaduni huo.
Kuna mambo mazito yamefanyika nchini bila ya kura ya maoni. Mifano ni kama Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964; kuletwa mfumo wa chama kimoja mwaka 1965; Azimio la Arusha la mwaka 1967 na sheria zilizofuatia za kutaifisha mali; kuja kwa mfumo wa vyama vingi wa 1992, na kadhalika.
Ingekuwa kumepigwa kura ya maoni mwaka 1991 na wananchi asilimia 80 wakakataa mfumo wa vyama vingi, kama vile takwimu za Tume ya Nyalali zinavyoonyesha, kwa matokeo hayo si tungekataa mfumo wa vyama vingi? Athari zake tunazijuwa? Suala gani wataulizwa wananchi katika kura hiyo ya maoni; ikiwa wanataka au hawataki serikali ya mseto. Mimi nafikiri kwamba ‘Kamati ya Mwafaka’, baada ya kutafakari matatizo yote yaliyojitokeza tangu uchaguzi wa 1995, na zile chaguzi za 2000 na 2005, wakaonelea kwamba njia ya busara ni kuwa na serikali ya mseto.
Kama alivyosema Rais Jakaya Kikwete na Profesa Ibrahim Lipumba, kila upande katika kamati hiyo imekuwa ikishauriana na wakuu wake. Hii ni kusema kwamba Rais Kikwete, Rais Amani Karume na Profesa Lipumba wote walijua nini kimezungumzwa katika kamati hiyo na nini kimekubaliwa.
NEC ya CCM na Baraza Kuu la CUF vyote vilikuwa vikiarifiwa nini kinatokea. Mbona wakati wote huo wazo la kura ya maoni halikuletwa? Na baada ya Rais Karume kulileta suala hilo kwa Komredi Kingunge Ngombale Mwiru, Luteni Yusuf Makamba na Ali Ameir Mohamed, ambao ni wajumbe wa ‘Kamati ya Mwafaka’, si wangerejea kwa wenzao wa upande wa CUF kuwasikiliza wana maoni gani, kabla ya jambo hilo kupelekwa kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM?
Tafsiri iliyojitokeza sasa hivi ni kwamba CCM haitaki hata hiyo dhana ya serikali ya mseto, na kusema kuwe na kura ya maoni ni njia tu ya kistaarabu ya kukataa jambo hilo. Kwani hata utekelezaji wake ambao unataka mabadiliko ya kikatiba, kuandaa daftari la wapiga kura na uendeshwaji wa hiyo kura ya maoni sioni vipi itawezekana kufanyika na halafu tuwe na uchaguzi wa mwaka 2010. Mimi sioni kwamba kutakuwa na kura ya maoni na wala kama kweli kutakuwa na jitihada za dhati za kuiangalia upya Katiba ya Zanzibar na kubadilisha sheria ya uchaguzi na kuifuma upya Tume ya Uchaguzi ili kuhakikisha kwamba kutakuwa kweli na uchaguzi huru na wa haki. Na ikiwa hayo hayakufanyika haraka, basi itakuwa tunaelekea pabaya huku tukijua na tukiwa macho wazi!

1. Je, unadhani CCM inayo dhamira ya kweli ya kuleta maelewano ya kisiasa Zanzibar?

JIBU: Tunachoweza kusema juu ya CCM ni kutokana na dhamira zake za dhahiri, katiba yake na yale ambayo viongozi wake wanayazungumza hadharani. Na ikiwa chama hicho kinataka kubaki madarakani, Bara na Visiwani, na kuendelea kupata uhalali wa kuwa chama cha siasa, basi lazima kiende na wakati na kijifunze kutokana na historia ya nchi yetu lakini pia tujifunze kutokana na yanayotokea kwa wenzetu. Mizozo, uhasama, chuki, malumbano yasiyo na mwisho, uvunjwaji wa haki za binadamu, n.k., sio vitu vinavyowaunganisha watu bali vinaigawa jamii. Na jamii iliyogawanyika haipati maendeleo. La umuhimu pia ni urithi gani ambao Rais Jakaya Kikwete na Rais Amani Karume wanataka kuwaachia Watanzania baada ya uongozi wao?

2. Wachambuzi wanasema kuwa wahafidhina wa siasa za Zanzibar wanaogopeshwa na kipengele cha mgawanyiko wa madaraka. Je, hofu yao ina mashiko?

JIBU: Kwa jinsi maelezo yanavyoonyesha juu ya nini kimetokea katika Kamati Kuu na NEC ya CCM, sio suala la wahafidhina au wapenda maendeleo kushinda, lakini ni ukosefu wa uongozi. Inaonyesha katika suala hili Kamati Kuu haikwenda kwenye NEC na msimamo mmoja na kujua nini wanataka. Wachunguzi wengi wanasema kuwa mgawanyiko uliotokea haukupata kuonekana tangu mkutano mkuu wa TANU wa mwaka 1958 kule Tabora kuhusu kura tatu. Uongozi ni kuonyesha njia; na ili kufanya hivyo uongozi lazima uwe unajua wapi unataka kuwapeleka watu na kuamini kwamba utaweza kuwafikisha huko.

3. Kwa maoni yako, unadhani nini kingeanza, kura ya maoni au mazungumzo? Na je, kwani makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo hayawezi kupewa uhalali wa kisheria mpaka wananchi washiriki katika kura za maoni?

JIBU: Ninavyofahamu mimi ni kwamba ile Rasimu iliyotolewa na “Kamati ya Mwafaka’ na kupelekwa kwenye vyombo vya juu vya CUF na CCM ilimaanisha kwamba mazungumzo yamemalizika na kilichohitajika ni ridhaa ya vyombo hivyo na utekelezwaji wa mapendekezo hayo. Utekelezwaji ungeweza kufanyika kwa kulitumia Baraza la Wawakilishi, na hata pale ambapo ridhaa ya thuluthi mbili ya wajumbe ingehitajika, hilo lisingekuwa gumu kwa vile jambo hilo litakuwa limekubaliwa na vyama vyote viwili.

4. Hoja nyingine inayotolewa na wanasiasa wa vyama vingine (visivyo CUF na CCM) ni kuwa mazungumzo yangeshirikisha vyama vyote vya siasa na wala si CUF na CCM pekee, wewe unaonaje hoja hiyo?

JIBU: Ni hoja sahihi kabisa. Na si vyama vya kisiasa, bali pia asasi zisizokuwa za kiserikali, jumuiya za kidini, vyama vya kitaalamu, watu mashuhuri katika jamii, n.k. Kwani kinachotafutwa ni mustakabali wa taifa zima na kila mmoja ni mdau katika hilo. Lakini hili lingekuja katika awamu ya pili. Kuna mambo yaliyokubaliwa katika Mwafaka I na II ambayo hayakutekelezwa; kuna yale yaliyojitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2005 ambapo ilipelekea CUF kusema hawamtambui Rais Amani Karume, na mengineyo. Sasa haya ni ya CUF na CCM. Matumaini yangu mimi ni kwamba ikiwa mwafaka utafikiwa, utatoa fursa ya kuwa na mjadala mpana zaidi na wa kitaifa kuhusu mustakabali wa taifa; na hapo kila chama, jumuiya, taaluma, n.k., ingebidi vishirikishwe.

5. Je, uamuzi wa CUF kujitowa katika mazungumzo ya Mwafaka ni sahihi?

JIBU: Bila ya shaka CUF ina sababu zake za kufanya hivyo. Rasimu ile iliyokubaliwa na Kamati ya Mwafaka imejengeka kwenye msingi kwamba kurekebishwa kwa katiba, kufumwa upya kwa Tume ya Uchaguzi, kufanyiwa marekebisho ya sheria ya uchaguzi na kutengeneza mazingira ya kuwapo kwa uchaguzi wa haki na huru, vitafanyika kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010; na chombo kitakachosimamia haya ni serikali ya mseto. Sasa kwa CCM kuleta jambo jipya la kura ya maoni na kutamka wazi kwamba kwa maoni yake serikali ya mseto itakuja baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 imekuwa kwamba ule msingi wa makubaliano yale haupo tena.

6. Pamoja na kususia mazungumzo, unadhani CUF inaweza kuchukuwa hatua gani zaidi katika kukabiliana na usanii wa kisiasa wa CCM?

JIBU: Huu sio usanii, ni mbinu za kisiasa. Utakumbuka katika taarifa iliyotolewa na Makamba, Ngombale na Ali Ameir kwenye Kamati Kuu ya CCM walizungumzia kwamba kuleta kura ya maoni ni njia ya ‘kuipiku’ CUF! Kutopatikana kwa suluhisho la kudumu sio kwamba inaiumiza Zanzibar tu lakini athari zake zinafika Bara pia. Tumeona vipi tatizo hili la Zanzibar lilivyochukuwa mjadala mkubwa na mrefu kwenye vikao vya CCM huko Butiama. Ikiwa tutafikia uchaguzi wa mwaka 2010 bila ya tatizo hili kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, nachelea kufikiri nini kitatokea. Hiki si kitisho bali ni baada ya kuangalia nini kinatokea nchini na kuona pia vipi mambo yanavyokwenda ulimwenguni.

8. Maalim Seif aliripotiwa kuwa alikwenda Uingereza na nchi za Scandinavia kuwashawishi waingilie kati suala la Mwafaka. Je, hatua hiyo aliyoichukuwa ni sahihi? Kama ni sahihi, je unadhani nchi hizo wahisani zinaweza kufanya nini katika kufikia hatima ya mgogoro wa kisiasa Zanzibar?

JIBU: Sijui Maalim Seif alikwenda wapi na kufanya nini. Lakini ninachojua ni kwamba jumuiya ya mabalozi wa kigeni hapa nchini imekuwa ikifuatilia kwa karibu mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika baina ya CCM na CUF, na wengi wao wamesikitishwa na yaliyotokea. Nini watashauri serikali zao sijui, lakini matamshi aliyotoa Balozi wa Marekani hivi karibuni yanaashiria kwamba mambo hayatokuwa shwari si kwa Zanzibar tu bali kwa Tanzania kwa ujumla. Seif Shariff kokote atakakokwenda atasikilizwa lakini sidhani kwamba siasa za nchi hizo kwa Tanzania zitategemea nini Seif anataka bali hali halisi ilivyo nchini na maslahi ya nchi hizo.

9. Unazitathmini vipi jitihada za Rais Jakaya Kikwete katika kuondosha mpasuko wa kisiasa Zanzibar?

JIBU: Rais Jakaya Kikwete alitamka azma yake ya kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar alipohutubia Bunge kwa mara ya kwanza kama Rais mwezi Desemba 2005. Viongozi wengi wa kiafrika hawana utamaduni wa kujali vipi historia itawasema na kuwahukumu katika kipindi cha utawala wao au wanataka kuwacha urithi upi ambao ukumbukwe wa utawala wao. Kuweza kulitanzuwa tatizo hili la Zanzibar sio tu kutampa Rais Kikwete na Rais Karume heshima zaidi nchini na kimataifa lakini pia itakuwa wamewacha urithi mzuri.

10. Nini maoni yako kuhusu hisia za Wapemba kwamba wanataka waachiwe kisiwa chao na waunde serikali yao?

JIBU: Kwa upande mmoja naweza kufahamu kwanini hisia kama hizo zinaibuka sasa, lakini kwa kweli ni mawazo ya hatari kwa taifa letu. Ni kitu ambacho Mwalimu Nyerere alituonya kabla. Leo Wapemba wanaweza kujiona kuwa ni kitu kimoja dhidi ya Waunguja, lakini kesho itakuwa ni wale kutoka Ziwani, Kengeja, Wete au Kisiwa Panzi. Hoja sio kujitenga bali kujitahidi kujenga demokrasia ya kweli ambapo kila mmoja atakuwa na hisa katika upanuwaji wake, kuenziwa kwake na kudumishwa kwake. Haya ni mapambano ambayo wapenda demokrasia na amani lazima washinde!

KUHUSU MIMI

JINA:Hawra Shamte
MAKAZI:Dar es salaam
NCHI:Tanzania
KAZI:Mwandishi

KUELEKEA BUNGE LA BAJETI 2006

QuickTopic free message boards
Bonyeza hapa ili uweze kuelezea: NINI MTAZAMO WAKO JUU YA BAJETI IJAYO YA MWAKA 2006/07 NCHINI TANZANIA?

VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI

 • The Citizen
 • Mwananchi
 • Mwanaspoti
 • Business Times
 • Majira
 • Daily News
 • Nipashe
 • The Guardian
 • The Express
 • Kiongozi
 • Uhuru/Mzalendo
 • Arusha Times
 • BLOGI ZA KISWAHILI

 • Bangaiza
 • Mwandani
 • Pambazuko
 • Damija
 • Mtafiti
 • Martha
 • Gaphiz
 • Swahili time
 • Miruko
 • Dira yangu
 • Msangimdogo
 • Jeff Msangi
 • Kasri la mwanazuoni
 • Kurunzi
 • Baragumu
 • Mawazohuru
 • Fikra Thabiti
 • Mtandaoni
 • Motowaka
 • Mkwinda
 • Ngurumo
 • Nyembo
 • Bwaya
 • Omega
 • Tafakari za Maisha
 • Nuru akilini
 • Mtandawazi
 • Mhujumu
 • Vijimamboz
 • Wakati wa Ukombozi
 • Kijiwe Joto
 • Watoto Wetu
 • Jungu kuu
 • Kisima cha Weledi
 • Jarida la Ughaibuni
 • Bhalezee
 • Sauti ya Baragumu
 • Kona yangu
 • Furahia Maisha
 • Bakanja
 • Terrie Swai
 • Fatma Karama
 • Kazonta
 • Binti Afrika
 • Blogu ya Kilimo
 • Ukombozi
 • Mwafrika
 • Digital Africa
 • Blogu ya lugha mseto
 • BLOGI ZA WAAFRIKA

 • BLOGAFRICA
 • BLOGU ZA WAAFRIKA
 • DIGITAL AFRICA
 • MAMA JUNKYARD'S
 • MSHAIRI
 • KENYAN PUNDIT
 • MONGI DREAMS
 • ISARIA MWENDE
 • CUNNING LINGUISTICA
 • ETHIOPUNDIT
 • MOCHALICIOUS
 • UNGANISHA
 • DEMOKRASIA KENYA
 • CHANUKA
 • BANKELE
 • MAARIFA/AKIEY
 • AFROMUSING
 • NEHANDA DREAMS
 • BLACK LOOKS
 • YUMMY WAKAME
 • AFRICAN OIL POLITICS
 • NUBIAN SOUL
 • SANAA
 • VIRTUAL INSANITY
 • MENTAL ACROBATICS
 • KENYA UNLIMITED
 • JIKUMBUSHE KAZI ZANGU ZA ZAMANI

  April 2006 May 2006 June 2006 October 2007 November 2007 December 2007 May 2008 July 2008 October 2008 July 2009 August 2012 October 2012

  Imetengenezwa na

  Ukibofya hapa utapelekwa katika Blogi ya msangimdogo

  na inawezeshwa na