" Jamii iliyostaarabika ni yenye kuheshimu Mawazo & Mitazamo ya wengine. Mchango wako katika kazi yoyote ulenge kujenga jamii yenye Kujitambua, Kujithamini na Kujiwajibisha "

 
Wednesday, November 28, 2007

 Adui yako muombee njaa, akikosea kidogo kandamiza!

WALIOSEMA siasa ni mchezo mchafu, leo nami naungana nao kuyaamini maneno yao. Kweli siasa ni mchezo mchafu!

Wanasiasa daima hubuni stratejia mpya za kujipatia maslahi ya kisiasa, mbinu, mikakati iliyopo katika siasa hasa za ushindani ni jinsi gani chama kimoja kitakavyokigaragaza kingine katika medani za kisiasa, iwe ni kwa majigambo, majibizano, kashfa na hata kubadilisha mwelekeo wa duru za siasa za wakati husika.

Kwa kawaida katika vyama huwa na idara na maofisa maalum wa propaganda, hawa ni makuhani wa propaganda, wamekubuhu, waweza kukushawishi kwamba hivi sasa ni usiku ilhali ni mchana, kisa kuna wingu limetanda.

Propaganda ni utaalamu ambao kwa Tanzania, kinara wake ni Chama Cha Mapinduzi hawa wana ujuzi wa kutosha katika masuala ya propaganda na ujuzi huo si wa kubabaisha, una mashiko ya Urusi na Quba mabingwa wa propaganda za kijamaa duniani.

Chochote kinachotendeka katika medani za siasa hakishangazi, na ndiyo maana sikushangaa kumsikia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Taifa, Jakaya Kikwete alipokuwa akifungua tawi la CCM litakalowahudumia wanachama takriban 700 ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu vya Kampala na Makerere, mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, “hali ya kisiasa nchini ni shwari, hizo kelele kelele wanazozisikia ndio siasa, hivyo zisiwape shaka, adui yako muombee njaa, akikosea tu, kandamiza hapo hapo, si mnasikia tunavyokandamiza...” Sehemu ya hafla hiyo kwa bahati ilionyeshwa na Televisheni ya Taifa.

Kumbe, hivi vilio vinavyotolewa na wananchi na wanasiasa kuhusu Buzwagi, Richmond na vinginevyo ni ‘kelele kelele’ tu za kisiasa? Kelele ambazo si hasha kutomzuia mwenye nyumba kulala.

Je ni vipi tutaidadavua kauli hii ya Mwenyekiti wa Chama Dola nchini? Je anataka kutueleza nini hasa? Kelele zinazopigwa siku za hivi karibuni ni suala la kuchunguzwa mikataba inayoingiwa na Serikali kama ile ya madini na ile ya nishati ya umeme.

Mbunge kijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe aliamsha hamasa mpya pale alipoliomba Bunge liunde kamati huru ya kuchunguza uingiaji wa mkataba wa machimbo ya madini katika mgodi wa Buzwagi. Yaliyotokea kwa Zitto ni historia, lakini nini baadaye Rais alifanya?

Alimteua Zitto kuwa mjumbe wa Kamati ya Madini. Waswahili wana msemo usemao kuwa ‘mchawi mpe mtoto alee,’ msemo huo ukasadifu kwa Zitto kupewa kazi ya muda ya kulea mtoto, ni mjumbe wa Kamati ya Madini, alichotaka Zitto kukitoa kikoa, sasa hakitoleki tena, akijaribu tu ni yeye ndiye atakayepelekwa ‘msukule.’

Mapigo ya CCM si ya kitoto, ni ya kisayansi, hawakurupuki bali hufanya hesabu na mara nyingi jawabu zake huwa sahihi.

Badala ya watu kujadili jinsi mikataba ya madini isiyolinufaisha taifa inavyoingiwa, sasa wanamjadili Zitto, kwanini wee, kwanini. Kwani vipi jamani? Kwani wao wananchi wanataka iwe vipi?

Ingelikuwa Rais hakuiteua kamati ile kwa jinsi alivyoiteua angelaumiwa, ameiteua walioteuliwa wanalaumiwa, kwani jamani Zitto kosa lake nini?

Wako waliozikaanga mbuyu, sasa wanawaachia wenye meno watafune. Huo ndio mchezo wa siasa, hautabiriki, haufahamiki.

Haya Rais huyu huyu, wiki tatu zilizopita alilikoroga togwa, alisema kuwa suala la Mahakama ya Kadhi si sera ya CCM wala msimamo wa Serikali yake, tena Rais kenda kuyazungumzia hayo kwenye jukwaa la Kanisa, wakati wa kumsimika Mkuu mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa. Jambo hilo liliwakera Waislam, walikereka hasa kutokana na hadhira aliyoitumia Rais kuwasilisha ujumbe huo mzito, unaowahusu Waislam.

Binafsi sidhani kama Rais aliyafanya hayo kibubusa, bila shaka alikuwa na sababu zake maridhawa. Lakini nisichokitambua ni kuwa je ile nayo ni siasa?

Kwa kuwa siasa ni uongo na mchezo mchafu, yawezekana ahadi ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi ni ahadi ya uongo wa kisiasa, tuliisikia ikitolewa katika majukwaa ya kisiasa wakati wa kampeni za mwaka 2005, ahadi hiyo hiyo ambayo leo twaambiwa kuwa si sera ya CCM ndiyo iliyotumika kumnadi mgombea wa Urais wa CCM mwaka 2005, tena ilikuwa ikisisitizwa sana katika maeneo yenye Waislam wengi.

Vipi ahadi ile iliingia katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005, wananchi hawana shida ya kufahamu ila wanafahamu kwamba ipo na kama ilivyo kwa ahadi nyingine zote zilizotolewa wakati wa Kampeni ama zile zilizoingizwa katika ilani, wananchi wangependa ahadi hiyo itekelezwe.

Kama haiwezekani waelezwe mazingira yaliyosababisha kushindwa kuitekeleza ahadi hiyo, lakini kuwaambia wananchi kuwa hiyo si sera ya CCM wala ya Serikali ni kuwacheza shere Wapigakura.

Kwa mtindo huu wa Rais, nadhani hizo alizoziita kelele za kisiasa zitaendelea kupigwa kila uchao na kwa uchache wangu wa nadhari, nafikiri kelele hizi si nzuri, si za afya katika siasa na iko siku Rais zitamgharimu.
hshamte@mwananchi.co.tz

Tuesday, November 27, 2007

 Hayawi hayawi, yamekua.

Comrades

Huu n i uchambuzi uliotoka Nov 3 kwenye gazeti la Mwananchi, lakini kwa vile kuna wana blog walioniomba niupandishe wavuni, ndio kwanza leo napata nafasi ya kuupandisha, bcs nilikuwa na matatizo ya kifamilia kidogo.
Nawatakia kila la heri na naomba muudadavue, si huu tu na mingine mingi ambayo nitajitahidi kuwaletea kila mara.
Wasalaam
Mnyongemnyongeni lakini haki yake mpeni

Kila la heri CCM, tunatarajia mabadiliko ya kimaendeleo

HAYAWI hayawi, leo yanakuwa, ile siku waliyokuwa wakiisubiri kwa hamu leo imefika. Si ya ndirimo na vifijo pekee, bali pia ya wasiwasi na huzuni.

Ifikapo kesho, mbivu na mbichi itakuwa imejulikana. Wako watakaofurahi na wako watakaotamani ardhi ipasuke, wajifukie. Lakini yote hayo ni maisha, kuna kupata na kukosa.

Masikio ya Watanzania wote leo na kesho yameelekezwa Dodoma, yanataka kusikia kinachojiri. Hayo yanatokea kwa sababu kubwa moja, Chama kinachofanya uchaguzi wake wa ngazi za juu za uongozi, ni Chama Dola, utake usitake kitakugusa kwa sababu Serikali inatekeleza sera za Chama Cha Mapinduzi.

Kuvunda kwa uongozi ndani ya CCM ni kuvunda kwa Serikali. Tunatarajia kuwa wana-CCM watatuchagulia viongozi bora, makini na ambao kweli wanayo ari, nguvu na kasi ya kuwafikisha Watanzania kwenye nchi ya ahadi, watakakokwenda kula Manna na Sal-wa.

Wamesema wasemao kuwa Chama fisadi, huzaa Serikali fisadi. Kete za Watanzania zimelala kwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, je ataweza kubadilisha mwelekeo wa Chama? Je Kikwete ataweza kukinusuru Chama na ufisadi?

Yote hayo yanategemea sana timu itakayochaguliwa na Mkutano huu mkuu, sambamba na uteuzi wa atakaowateua Mwenyekiti. Tunawaomba watuletee watu safi! Wenzetu, watakaojali maslahi yetu. Chonde chonde, wajumbe msituangushe!

Napenda kuungana na wale wasemao kuwa pengine tatizo lililopo katika utekelezaji wa sera za CCM ni timu iliyopo, si msaada kwa Mwenyekiti. Mwenyekiti anahitaji kushauriwa na si kuogopwa. Anapaswa apewe mrejesho-nyuma kuhusu maoni ya wananchi, huyu hastahili kudanganywa, anapodanganywa maana yake ni kuwa wanaodanganya, wanawadanganya wananchi. Huyu ni mwakilishi wa wananchi, wamemkasimia madaraka yao, awasimamie mustakabali wao na wa nchi yao. Mambo yakienda shaghala-baghala, wanaokomolewa ni wananchi na kamwe si Rais na Mwenyekiti wa Chama Dola.

Kwa mara nyingine tena, wana-CCM tunawaomba mtuchagulie watu makini, wenye uchungu na nchi hii, tunaomba mtupe watu watakaomsaidia Mwenyekiti.

Tunafahamu kwamba kibarua kilichoko mbele yenu, si haba, lakini tunawasihi kwamba mnapotoa maamuzi yenu yasiwe ni yale yaliyoshawishiwa na ‘vipeperushwa.’ Vifanyieni kazi vipeperushi na mtuchagulie viongozi bora.

Inashangaza kuona kwamba watu wanakimbilia mzigo wa dhamana, je hawauogopi? Au kipo wanachonufaika nacho? Ikiwa dhamana ina faida, tunaomba tugawane sote, sote tunufaike na rasilimali za nchi hii.

Kadhalika tunawaomba wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, kusaidia kuweka mwelekeo wa Chama, kwani wako wanaosema kuwa CCM imepoteza mwelekeo. Wako wanaosema kuwa slogani ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya si dira ya Chama, bali ni slogani tu kama ilivyo ile ya ‘Maisha Bora kwa kila Mtanzania.’ Hizo slogani zinafaa kuwekewa mikakati ili ziwe dira, kama ilivyokuwa wakati wa sera za ujamaa na kujitegemea. Mwelekeo wa CCM ulikuwa ni kuwatetea wanyonge, wakulima na wafanyakazi. Mweleko huo uko wapi sasa?

Taswira ya CCM ya leo, haionyeshi mwelekeo huo adhimu, leo hii Chama kimejitoa kutoka cha kutetea haki za wanyonge na sasa kimekuwa ni cha kutetea hali za ‘kundi maslahi.’ Hoja yangu si kutokuchagua matajiri, bali ni kuwa na watu wanaothamini shabaha ya kuundwa kwa CCM.

Sisi wananchi tumechoshwa na CCM ya ‘Chukua Chako Mapema,’ tunataka kuona Mapinduzi ya kimaendeleo, CCM isaidie kututoa kutoka katika hali duni na kutufikisha katika hali bora. Tunatarajia CCM itufikishe katika nchi ya ahadi, yenye matunda na mafanikio tele.

Je, si kweli kwamba hohehahe leo ni vigumu kupata uongozi ndani ya CCM? Je yawezekana kweli kupata kura, bila ya wewe kutoa kula kwanza? Takukuru mna kazi, kwani hongo hutolewa gizani! Wapi mtawaona, wapi mtawakamata? Wale mnaofanikiwa kuwakamata mnawakamata kama kafara tu, na nina wasiwasi kwamba mnahangaika kukamata vibua wakati mapapa yamejizamisha katika bahari kuu! Kama wao wanapiga mbizi, nanyi mnapaswa mzamie mbizi na kama wao wanapiga kasia, nanyi tumieni kasia ili mwende kasi inayostahili, muwafikie na muwakamate.

Mwisho naomba nitoe kisa kimoja ambacho kina mazingatio, kisa hiki napenda kukitoa kama zawadi maalum kwa Mwenyekiti wa CCM.

‘Nabii Ibrahim siku moja aliamua kumtembelea mwanawe Ismail, kule jangwani alikomwacha na mama yake Haajirah. Alipofika hakumkuta Ismail alikuwa kaenda kuwinda, safari hiyo kwa kawaida ilikuwa ikimchukua zaidi ya mwezi, lakini kwa bahati Nabii Ibrahim alimkuta mka-mwana wake, baada tu ya kumkaribisha bila ya hata kumtambua mgeni yule ni nani, mkewe Ismail akaanza kuelezea matatizo yanayowakumba katika kijiji kile, ooh! Hapa tuna shida ya maji, kitoweo mpaka tuhangaike…

Nabii Ibrahim alikaa pale kwa mwanawe siku alizokaa, alipoondoka akaacha maagizo; ‘Akija mumeo, mwambie nyumba yake nzima, lakini kizingiti chake kibovu!’ Ismail alipopata ujumbe ule akamwambia mkewe kuwa, huyo ni baba yangu, amenipa maagizo kwamba mke niliyenaye hafai, hivyo nakuacha!

Kwako Mwenyekiti; Nyumba yako ni nzima, lakini kizingiti chako kibovu!

Hawra Shamte ni Mhariri wa Siasa wa Gazeti la Mwananchi.

hshamte@mwananchi.co.tz
0754 849694

KUHUSU MIMI

JINA:Hawra Shamte
MAKAZI:Dar es salaam
NCHI:Tanzania
KAZI:Mwandishi

KUELEKEA BUNGE LA BAJETI 2006

QuickTopic free message boards
Bonyeza hapa ili uweze kuelezea: NINI MTAZAMO WAKO JUU YA BAJETI IJAYO YA MWAKA 2006/07 NCHINI TANZANIA?

VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI

 • The Citizen
 • Mwananchi
 • Mwanaspoti
 • Business Times
 • Majira
 • Daily News
 • Nipashe
 • The Guardian
 • The Express
 • Kiongozi
 • Uhuru/Mzalendo
 • Arusha Times
 • BLOGI ZA KISWAHILI

 • Bangaiza
 • Mwandani
 • Pambazuko
 • Damija
 • Mtafiti
 • Martha
 • Gaphiz
 • Swahili time
 • Miruko
 • Dira yangu
 • Msangimdogo
 • Jeff Msangi
 • Kasri la mwanazuoni
 • Kurunzi
 • Baragumu
 • Mawazohuru
 • Fikra Thabiti
 • Mtandaoni
 • Motowaka
 • Mkwinda
 • Ngurumo
 • Nyembo
 • Bwaya
 • Omega
 • Tafakari za Maisha
 • Nuru akilini
 • Mtandawazi
 • Mhujumu
 • Vijimamboz
 • Wakati wa Ukombozi
 • Kijiwe Joto
 • Watoto Wetu
 • Jungu kuu
 • Kisima cha Weledi
 • Jarida la Ughaibuni
 • Bhalezee
 • Sauti ya Baragumu
 • Kona yangu
 • Furahia Maisha
 • Bakanja
 • Terrie Swai
 • Fatma Karama
 • Kazonta
 • Binti Afrika
 • Blogu ya Kilimo
 • Ukombozi
 • Mwafrika
 • Digital Africa
 • Blogu ya lugha mseto
 • BLOGI ZA WAAFRIKA

 • BLOGAFRICA
 • BLOGU ZA WAAFRIKA
 • DIGITAL AFRICA
 • MAMA JUNKYARD'S
 • MSHAIRI
 • KENYAN PUNDIT
 • MONGI DREAMS
 • ISARIA MWENDE
 • CUNNING LINGUISTICA
 • ETHIOPUNDIT
 • MOCHALICIOUS
 • UNGANISHA
 • DEMOKRASIA KENYA
 • CHANUKA
 • BANKELE
 • MAARIFA/AKIEY
 • AFROMUSING
 • NEHANDA DREAMS
 • BLACK LOOKS
 • YUMMY WAKAME
 • AFRICAN OIL POLITICS
 • NUBIAN SOUL
 • SANAA
 • VIRTUAL INSANITY
 • MENTAL ACROBATICS
 • KENYA UNLIMITED
 • JIKUMBUSHE KAZI ZANGU ZA ZAMANI

  April 2006 May 2006 June 2006 October 2007 November 2007 December 2007 May 2008 July 2008 October 2008 July 2009 August 2012 October 2012

  Imetengenezwa na

  Ukibofya hapa utapelekwa katika Blogi ya msangimdogo

  na inawezeshwa na