Mzimu wa Muungano tusipoutuliza utatukosesha amani
MAFAHALI wawili wakipigana ziumiazo nyasi. Huo ni msemo maarufu wa Kiswahili ambao bila shaka una maana pana. Hivi sasa hapa kwetu kuna mafahali wawili wapiganao, yeyote yule atakayebwagwa au hata ikiwa kila mmoja mwisho wa siku atashika njia yake, lakini ni wazi kwamba nyasi zitakuwa zimegaragazwa. Suala la mafuta ambayo yanadaiwa kuwapo Zanzibar limegeuka mzimu unaokuja na kuondoka, lakini hivi sasa unaonyesha kana kwamba umeamua kubaki kwetu, unatukokoteza, unaturudisha nyuma, unatutia wahka. Kwa kawaida mzimu wowote hutulizwa, hivyo ili na huu usiendelee kutuandama tunapaswa kutafuta njia za kuutuliza, kinyume cha hivyo utatukosesha amani. Suala hili limekuwa likiibuka mara kwa mara kwa sababu tu kwa muda wote limekuwa likishughulikiwa kwa udanganyifu, inaonyesha kana kwamba katika kamati ya kushughulikia kero za Muungano inayoongozwa na Makamu wa Rais wajimbe wakiwemo, Waziri Mkuu kwa upande wa Bara na Waziri Kiongozi kwa upande wa Zanzibar, kuna watu ambao wanaogopana, au labda kuna upande unaouogopa mwingine na kushindwa kuambizana ukweli na kinachobaki ni kutoa ahadi za kisiasa tu zisizo na mwisho, “suala hili tunalishughulikia,” siku zinakwenda, miezi inapita, miaka inakatika, awamu zinabadilika, ahadi hiyo bado ingalipo. Mara hii Wazanzibari wameamua kumtafuna jongoo kwa meno. Kasimama Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mansour Yusuf Himid mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Mkuu wa Shughuli za Serikali ndani ya Baraza, Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha akiwapo na akiwa kimya kumsikiliza. Kwa sauti kubwa na ya hamasa, Himid akasema ‘Wazanzibari tumechoka kuburuzwa katika suala hili, sasa huu ni uamuzi wa Baraza la Mapinduzi kwamba mafuta tunayatoa rasmi katika mambo ya Muungano…” Kiongozi wa mambo ya Serikali Barazani yuko pembeni kaketi, kimya kanyamaza, anang’aa ng’aa macho tu. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba Himid kapata baraka zote kutoka kwa wakuu wake kulisema jambo hilo, maana yake ni kwamba sasa watu wanataka kupimana nguvu. “Hii ni serikali ya Mapinduzi ati! Ikiwa hawa wenzetu hawataki kuelewa hivyo, itabidi sasa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itumie uamuzi wa nchi za kimapinduzi katika kuliondoa suala la mafuta na gesi asilia kwenye orodha ya mambo ya Muungano…” Bara nako wakubwa wanasema yao, eti Wazanzibari wanajifurahisha, eti mwenye mamlaka ya kutoa jambo katika Katiba ya Muungano ni Bunge tu. Hee! Kasheshe!Mara hii hapatoshi! Huenda pakachimbika bila sululu. Wazanzibari sasa wameamua kulishughulikia suala la mafuta na pengine mambo mengineyo yaliyoongezwa katika orodha ya mambo ya Muungano kutoka kumi na moja hadi 22, ilikuwaje yakaongezwa? Kwa idhini ya nani? Katika vikao vipi? Hayo ni maswali yanayoulizwa na bado hayajapata majibu labda kwa sababu hakuna mjibuji au hayajibiki. Wazanzibari sasa wanasema katika hili watatumia ukaidi, na kwa ukaidi hawajambo! Kwa ubishi kama wenyeji wa Kigoma, ubishi wao hawishi, wako tayari kukata kole la mnazi ili kuhesabu nazi zilizomo kwa sababu walishindana idadi yake wakati kole likining’inia mnazini, sasa kupata uhakika ni lazima liangushwe ili nazi zihesabiwe watu wote wakiona, huo ndio ukaidi wanaotaka kuuanzisha Wazanzibari na kwa hili husahau tofauti zao za kisiasa, hivi sasa itikadi yao moja tu, Uzanzibari na haki yao katika Muungano, likimalizika hili wataurudia ubishi wao wa zamani ule wa CCM na CUF waliouweka pembeni. Hali hiyo inaonyesha kwamba viongozi wetu wameshindwa kulishughulikia suala hili, lakini kwa kuliacha hivi lilivyo kwa kila mwenye kinywa, sauti na nafasi kusema atakavyo, huenda lisitufikishe popote na badala yake kuzua mgogoro mkubwa au pengine tuseme kwamba sasa mgogoro wa kikatiba utaibuka na hautazimika mpaka zijulikane mbichi na mbivu. Mara kwa mara wataalamu wa masuala ya siasa wamekuwa wakipendekeza kwamba tatizo hilo lianze kutatuliwa katika chanzo chake na si katika matawi, tatizo ni Katiba na Mkataba wa Muungano au pengine tatizo ni Muungano wenyewe. Inashangaza kuona kwamba watawala hawataki na wala hawapendi mambo haya yaguswe, lakini ni vyema yakaguswa na kuzungumzwa leo kuliko kusubiri mpaka ukaidi na mabavu yatumike kwani kwa kuruhusu hayo kutokea, huenda tukagawana mbao! Hiyo ni kuonyesha kwamba subira ya wananchi wa Zanzibar sasa inakaribia kufikia kikomo na hiyo inadhihirishwa kutoka vinywani mwa wawakilishi wao, haya mambo si ya kuyafanyia mzaha kwani Waswahili wanasema; ‘Mzaha mzaha, hutumbuka usaha.’ Binafsi nadhani mpira huu wa masuala ya Muungano sasa unapaswa kuchezwa na wakuu wa nchi husika, wasiachiwe Mansour Himid na Adam Malima kurushiana pasi kali na kuziumiza nyasi, kwani hawa ni vijumbe tu, tunawaomba wahusika waingie uwanjani walisakate kandanda! Hawra Shamte ni Mhariri wa Siasa wa Gazeti la Mwananchi. hshamte@mwananchi.co.tz 0754 849694
Labels: mafuta
0 Maoni ya Wasomaji:
Post a Comment
<< Rudi mwanzo