Na watajwe ili wakome kutufisidi na kutufilisi
Hawra Shamte
NAKUBALIANA kwa asilimia 100 na ushauri wa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta kwamba waliohusika na kuhamisha fedha nchini na kuzipeleka nje ya nchi kuzificha watajwe. Nami naungana naye kushangaa kwa nini hawatajwi?
Nashangaa kwa sababu hii si silika ya Watanzania kunyamazia uovu au kutishika kuusema uovu au kuogopa kuwaadhiri waovu.
Kwanini waovu hawatajwi? Kwanini tumekuwa tukitishia tu kuwataja watu ambao tunasema tunao ushahidi wa kutosha kuwa wanaifisidi nchi, wanahawilisha rasilimali za nchi.
Wanaohamisha fedha nchini na kuzipeleka kuzihifadhi katika benki za nje, hata kama ni fedha zao na tujaalie kuwa wamezipata kihalali, lakini kimsingi hawa ni wahujumu wa uchumi wa nchi.
Ikiwa uchumi wa taifa masikini kama Tanzania unategemea mzunguko wa dola ya Marekani, inakuwaje mtu mmoja anachukua mamilioni ya dola (anayodai kuwa ni yake) na kwenda kuyaweka katika benki ya Uswisi au kwengineko kokote kulikovunjwa shoka mpini ukabaki?
Anachofanya ni kukandamiza mzunguko wa fedha nchini kwake na kwenda kuimarisha mzunguko wa fedha wa nchi zilizoendelea.
Hii ni tabia ya uchoyo na ulafi, ikiwa mtu umepata inakuwaje hutaki na mwenzako apate? Huyu angeweka mabilioni yake ya fedha nchini, si yangetusaidia wengi kama yalivyotusaidia mabilioni ya Kikwete?
Kwa sababu kinachofanyika ni kuongeza uwezo wa benki wa kukopesha wateja wake, kwa kuwa benki inakuwa na wateja wakubwa wanaoingiza fedha nyingi zinazokaa kwa muda mrefu bila kazi.
Pengine wanafanya hivyo kwa kuogopa sheria ya uhujumu uchumi, pengine wanafanya hivyo kwa kuogopa kuulizwa wamepata wapi hivyo ‘vijisenti.’ Lakini kama wamezipata fedha hizo kwa njia halali kwanini waogope?
Nadhani umefika wakati Watanzania tukatae kugawana umasikini, kama baadhi yetu wanao utajiri walioupata kwa nguvu zao, kwanini waogope kujidhihirisha kama wao wana fedha na kisha fedha zao waziweke pahali panapotambulika kisheria.
Hawa akili zao na roho zao ni mbaya kuliko wale waliokuwa wakifukia magunia ya fedha chini ya ardhi wakati wa uhujumu uchumi. Wanaofanya hivi bila shaka ni wezi, wanaogopa kugundulika kama wana mabilioni ya fedha wasiyoweza kuyaelezea jinsi walivyoyapata.
Lakini hii tabia ya kuficha ukweli haikuanza leo, wala si wabunge tu wanaohofia kuuweka wazi ukweli, kwani hata viongozi wetu kadhaa serikalini katika kadhia tofauti tumeshawasikia wakisema kuwa wahalifu wanawafahamu lakini wanawapa muda wajirekebishe.
Tumeshawahi kumsikia kiongozi akisema kuwa amepelekewa orodha ya wauza unga, lakini anawapa muda mpaka Krismasi, ikimalizika atawashughulikia...
Tumeshawahi kumsikia kiongozi akisema anawajua waliojichukulia na kujihodhia fedha za Madeni ya Nje za Benki Kuu (EPA) lakini akawapa muda wazirejeshe...
Hii imekuwa ndiyo tabia, yamekuwa ndiyo mazoea, umekuwa ndio utamaduni mpya tulioamua kuufuata; utamaduni wa kuwahifadhi waovu, utamaduni wa kutowataja wezi, utamaduni wa kuwaonea haya wahalifu, utamaduni wa kuwapa muda wajirekebishe.
Wengine wamejifunza utamaduni wa kuwavumilia wanaowachafua, lakini hili la kutowataja wanaofisidi mali ya umma, wanaohawilisha rasilimali za taifa, hapa tumekithiri ada!
Wanahamisha nyara za taifa, wanasafirisha mpaka wanyama tunawavumilia, tunawaangalia tu. Wanachimba madini yetu, wanatuachia mashimo yasiyozibika, sisi tupo tunawaangalia tu, eti tunajivunia amani na utulivu.
Ni amani gani aliyonayo mtu anayeishi kwa mlo mmoja kwa siku? Ni amani gani anayoipata mtu anayetafuta maji kuanzia saa nane za usiku mpaka saa 6 mchana, anasubiri chemchem ifumuke, achote kwa kata, tena kwa utulivu ili asiyachafue? Haya ndiyo maji anayotarajia kwenda kunywa yeye na familia yake. Anafanya hivyo kwa sababu ahadi ya kupelekewa maji hadi kwenye kaya yake bado haijatekelezwa kwa sababu Serikali haina fedha, lakini Serikali hiyohiyo inawaangalia baadhi ya wananchi wake na hata wawekezaji iliyowaalika waje nchini kuwekeza, wakihamisha rasilimali za taifa.
Ni utulivu gani anaoupata mama mjamzito ambaye katika zama hizi zenye maradhi ya kuambukiza ya kila aina, anapokwenda hospitalini kujifungua anakuta wanalazwa watatu katika kitanda kimoja?
Ni utulivu gani anaokuwa nao mwanafunzi wetu wa shule ya msingi pale anapoketi sakafuni na kuandika kwenye daftari lake hali ya kuwa amepinda mgongo na kukunja miguu?
Kwa hali hii ya kutodhibiti mali ya umma, hali ya kuwaacha wachache wakifaidi keki ya taifa, hali ya kuwaacha walafi wakikomba mboga yote na kuwaacha watoto wetu wakiwa na utapiamlo; kiasi kiongozi wetu aseme Tanzania ina rasilimali nyingi, lakini hajui kwanini bado ni masikini.
Atajuaje? Wakati wanayoyafanya hayo wanafanya kwa kificho? Wakati wanahamisha mamilioni ya fedha kwenda kuyaficha nje ya nchi kama wezi? Wakati watu hawako wazi na wala si wa kweli?
Masikini Tanzania imegeuzwa shamba la bibi, tena bibi mwenyewe keshafariki, shamba halina msimamizi, wajukuu wanajichumia hata vilivyo vichanga, visivyopea wanavipepea kwa moto, wanahamisha badala ya kula wao au hata kuwaruhusu wenzao kujichumia na kukidhi njaa, hamu na kuondosha ghamu zao. Hii ni hatari!
0655 849694
0 Maoni ya Wasomaji:
Post a Comment
<< Rudi mwanzo