" Jamii iliyostaarabika ni yenye kuheshimu Mawazo & Mitazamo ya wengine. Mchango wako katika kazi yoyote ulenge kujenga jamii yenye Kujitambua, Kujithamini na Kujiwajibisha "

 
Wednesday, August 22, 2012

Ajali ya Skagit: Haya ni matokeo ya taifa linalopenda mitumba


Hawra Shamte

Ilikuwa Septemba 10, 2011 ilipotokea ajali ya meli katika bahari ya Hindi, eneo la Nungwi Zanzibar.
Kumbukumbu na taswira bado hazijaondoka vichwani mwa Watanzania. Maumivu ya mioyo kila wanapowakumbuka vipenzi vyao, ndugu, jamaa na rafiki zao na hata Watanzania wenzao waliopoteza maisha katika ile ajali ya MV Spice Islander iliyoua zaidi ya watu 200.

Ajali ile ilituduwaza. Mengi yalisemwa, tafakuri nyingi zilidadavuliwa. Ingawa ajali haina kinga, lakini Waswahili wanasema tahadhari kabla ya athari.Tulidhani tumejifunza, au tumejirekebisha, lakini afanalek, ajali nyingine kama ile imetokea, Julai 18, 2012, tofauti ni aina ya meli na eneo meli ilipozama.

Kwa kawaida akipoteza maisha hata mtu mmoja kwa ajali zinazoweza kuzuilika, watu wenye akili murua lazima waingie simanzi, wajilaumu na waazimie kujikinga na ajali.

Tulidhani ajali ya Mv Spice Islander ilitupa fundisho, tuache kujaza abiria kwenye vipando. Tulidhani ajali ile ilitufunza kuchukua hatua za tahadhari zote zinazopaswa kuchukuliwa na vyombo vya majini. Tulidhani mamlaka husika zimetanabahi na kubaini makosa yanayotendeka katika sekta ya usafiri wa majini.

Tulidhani ripoti ya Tume iliyoundwa mara baada ya ajali ya Mv Spice Islander ingefanyiwa kazi badala ya kuwekwa kwenye majalada na juu ya mashubaka na kuziacha ziote vumbi, au kubaki kuwa historia isiyozingatiwa.

Tulidhani kwa kuwa tuliambiwa lililopita si ndwele, tungeganga yajayo, tatizo hili hata kama lingejirudia, lisingejirudia mapema hivi, angalau tungekuwa tumeliganga kidogo hata kama ikiwa hatukuliponya.

Mara hii ajali imetokea upande wa pili wa mkondo, imetokea katika mkondo wa Chumbe eneo la Pungume, kilomita 48 kutoka bandari ya Zanzibar.

Boti iliyozama mara hii ni Skagit inayomilikiwa na kampuni ya Seagull. Yenyewe pia ilibeba zaidi ya uwezo wake, yasemekana kuwa uwezo wake ni kubeba abiria 200. Yenyewe ilibeba watu 291 mbali na mizigo. Hadi jana Alhamisi taarifa zilisema kuwa waliookolewa walikuwa 142, waliopotea 113, waliopatikana wakiwa wamefariki ni 36. Kwa hesabu za harakaharaka ni kuwa watu takriba 150 wamejongomea.

Pamoja na maafa yote hayo, itakachofanya Serikali ni kuunda Tume ya kuchunguza chanzo cha ajali, je, inasaidia nini? Wakati tulipaswa kuunda Tume za kupanga mikakati ya jinsi ya kukinga ajali, lakini sisi tunaunda tume baada ya madhara kutokea.

Kwa kuwa sisi wanadamu ni wenye mazingatio, tulidhani Mv Spice Islander ingekuwa imetupa mazingatio, lakini masikini kwa vile sisi ni ‘zumbukuku,’ maisha yetu, taratibu zetu na mienendo yetu mibovu tuliendelea nayo kama kwamba hakuna kilichotokea, lililopita limepita.

Vyombo vyetu vingi vya uysafirishaji viko chini ya kiwango, kwa sababu kama ambavyo wengi wetu hatununui magari mapya, vilevile hatununui meli mpya wala ndege mpya, zaidi pia hatununui hata nguo mpya, tumeligeuza taifa letu kuwa taifa la mitumba, hizi tunazoziona sasa ndiyo athari zake.

Sisemi kama kipya hakizami (kwani Mv Titanic) ilizama ikiwa mpya wakati wa safari yake ya kwanza baharini. Lakini sote tunajua madhara ya vikuukuu, vijembe vilivyokongoka mpini, sisi tunavichukua na kuviweka vibanio.

Waswahili wanasema ukiumwa na nyoka hata ukiona unyasi utauogopa, lakini sisi hatuogopi nyoka wa aina yoyote yule, maisha kwetu kila siku yanakwenda kama kawaida, kwetu maisha ni mazoea si mabadiliko wala maendeleo.

Mwanzoni mwa miaka ya 70 wakati serikali zilipokuwa zikitoa huduma, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikuwa ikitoa huduma za usafirishaji. Ilirithi meli za Mv Afrika na Mv Jamhuri, zilipochakaa ilinunua meli ya Mv Mapinduzi na Mv Maendeleo. Aliyepanda Mv Mapinduzi na Mv Maendeleo atakuwa anafahamu jinsi zilivyokuwa. Zilikuwa meli kubwa, nzuri na madhubuti, hivyo usafiri wa baharini ulikuwa wa uhakika zaidi.

Baada ya serikali kuacha jukumu lake la kutoa huduma za usafiri, hivi sasa usafiri wa baharini kama ulivyo usafiri wa nchi kavu umekuwa shaghala baghala, kila mwenye mkweche wake anauingiza baharini au barabarani bila kujali kwamba anacheza na roho za watu.

Serikali zetu zipo, zimenyamaza kimya kama kwamba zinaridhika na hali inayoendelea. Kazi ya serikali sasa imekuwa ni kuboresha miundombinu ya barabara tu, haina habari ya vipando.

Waliopewa mamlaka ya kudhibiti vyombo vya usafiri nao kama wamelala usingizi, na hata kama wameamka, bila shaka wakiminyiwa mkono kwa makosa ya wasafirishaji, wao wanaufumbata. Hivyo makosa ya usafirishaji ni vigumu kumalizika nchini, kwa sababu Watanzania tumejifunza tabia ya kufumbia macho maovu.

Kama wameshtushwa kutoka usingizini, ati Sumatra jana (Alhamisi) ilikataza boti za asubuhi zisisafiri hadi zikaguliwe. Tahadhari inachukuliwa baada ya hatari, na hilo litafanyika kwa muda mchache tu, halafu Watanzania watazoea na watasahau, maisha yataendelea kama kawaida.

Tunaikumbuka hekaheka ya vidhibiti mwendo kwenye magari ya abiria, je, iliishia wapi? Baada ya hashuo kumalizika, kila msafirishaji akaendelea na mazoea, ajali zinatokea kama kawaida kwa sababu tunaamini kuwa ajali hazina kinga, lakini wakati huo huo tunatambua kuwa ziko tahadhari za kuchukua kabla ya ajali lakini sisi tunazipuuzia.

Taifa lina kilio, kwa bahati mbaya hakuna anayetuthibitishia kuwa Watanzania karibu tutapata maliwazo, karibu tutahaniwa vilio vyetu, kwani kama hazijaua 100 barabarani zinaua 200 baharini au 1000 majini. Ajali ya Mv Bukoba bado iko mawazoni mwetu, lakini tunaendelea kujipumbaza kama kwamba roho zilizopotea zilistahili kupotea.

Ajali zitokanazo na uzembe hazistahili kuwekewa maneno ya kuliwazwa, hizi ni lazima tuzipige vita kwa nguvu zetu zote, na hii haiko kwa wasafirishaji tu, hata kwa wasafiri; nao wanapaswa wachukue hatua za tahadhari, kama mtu ameliona basi limejaa, hata kama ana haraka, hana sababu ya kung’ang’ania kuingia katika basi hilo; hivyo hivyo kwa wapandaji boti na meli, kama abiria ametambua kuwa tiketi zimekwisha, hana sababu ya kung’ang’ania magendo kwani anapaswa atambue kuwa anaiweka roho yake rehani.

Tunayo mipango na mikakati mingi ya maendeleo, lakini kwa bahati mbaya mipango yetu karibu yote iko mbioni, hivi sasa hizi mbio zinapaswa zifike ukingoni. Tunataka kuona miumbombinu iliyo bora na nyenzo za usafiri zilizo imara, kinyume cha hivyo ni muhali kwa Watanzania kufuta machozi mashavuni mwao, mwaka nenda, mwaka rudi ajali zitatuliza!

0655 849694.

0 Maoni ya Wasomaji:

Post a Comment

<< Rudi mwanzo

KUHUSU MIMI

JINA:Hawra Shamte
MAKAZI:Dar es salaam
NCHI:Tanzania
KAZI:Mwandishi

KUELEKEA BUNGE LA BAJETI 2006

QuickTopic free message boards
Bonyeza hapa ili uweze kuelezea: NINI MTAZAMO WAKO JUU YA BAJETI IJAYO YA MWAKA 2006/07 NCHINI TANZANIA?

VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI

  • The Citizen
  • Mwananchi
  • Mwanaspoti
  • Business Times
  • Majira
  • Daily News
  • Nipashe
  • The Guardian
  • The Express
  • Kiongozi
  • Uhuru/Mzalendo
  • Arusha Times
  • BLOGI ZA KISWAHILI

  • Bangaiza
  • Mwandani
  • Pambazuko
  • Damija
  • Mtafiti
  • Martha
  • Gaphiz
  • Swahili time
  • Miruko
  • Dira yangu
  • Msangimdogo
  • Jeff Msangi
  • Kasri la mwanazuoni
  • Kurunzi
  • Baragumu
  • Mawazohuru
  • Fikra Thabiti
  • Mtandaoni
  • Motowaka
  • Mkwinda
  • Ngurumo
  • Nyembo
  • Bwaya
  • Omega
  • Tafakari za Maisha
  • Nuru akilini
  • Mtandawazi
  • Mhujumu
  • Vijimamboz
  • Wakati wa Ukombozi
  • Kijiwe Joto
  • Watoto Wetu
  • Jungu kuu
  • Kisima cha Weledi
  • Jarida la Ughaibuni
  • Bhalezee
  • Sauti ya Baragumu
  • Kona yangu
  • Furahia Maisha
  • Bakanja
  • Terrie Swai
  • Fatma Karama
  • Kazonta
  • Binti Afrika
  • Blogu ya Kilimo
  • Ukombozi
  • Mwafrika
  • Digital Africa
  • Blogu ya lugha mseto
  • BLOGI ZA WAAFRIKA

  • BLOGAFRICA
  • BLOGU ZA WAAFRIKA
  • DIGITAL AFRICA
  • MAMA JUNKYARD'S
  • MSHAIRI
  • KENYAN PUNDIT
  • MONGI DREAMS
  • ISARIA MWENDE
  • CUNNING LINGUISTICA
  • ETHIOPUNDIT
  • MOCHALICIOUS
  • UNGANISHA
  • DEMOKRASIA KENYA
  • CHANUKA
  • BANKELE
  • MAARIFA/AKIEY
  • AFROMUSING
  • NEHANDA DREAMS
  • BLACK LOOKS
  • YUMMY WAKAME
  • AFRICAN OIL POLITICS
  • NUBIAN SOUL
  • SANAA
  • VIRTUAL INSANITY
  • MENTAL ACROBATICS
  • KENYA UNLIMITED
  • JIKUMBUSHE KAZI ZANGU ZA ZAMANI

    April 2006 May 2006 June 2006 October 2007 November 2007 December 2007 May 2008 July 2008 October 2008 July 2009 August 2012 October 2012

    Imetengenezwa na

    Ukibofya hapa utapelekwa katika Blogi ya msangimdogo

    na inawezeshwa na